Apr 22, 2024 12:17 UTC
  • Vita vya Israeli dhidi ya Ghaza: Mkuu wa jeshi la Intelijensia ajiuzulu kubeba lawama aa shambulio la Hamas

Meja Jenerali Aharon Haliva, mkuu wa kitengo cha ujasusi cha kijeshi wa Israel, ametangaza kujiuzulu kwa sababu ya kushindwa kuzuia shambulio la kihistoria la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS la tarehe 7 Oktoba 2023.

Meja Jenerali Aharon Haliva amesema katika barua yake ya kujiuzulu nafasi ya mkuu wa kitengo cha kijasusi cha jeshi la Israel kwamba kitengo hicho hakikutekeleza jukumu lilichokabidhiwa.

Amesema, ninakiri kwamba tulifeli mno katika upande wa kijasusi na ndio maana HAMAS ilifanya shambulio kubwa dhidi yetu bila ya sisi kuonesha majibu ya haraka ya kuizuia HAMAS. 

Amedai kuwa waliona ishara za kufanyika shambulio la Oktoba 7 lakini ripoti zote zilipuuzwa na ngazi za juu zaidi za kijeshi na serikali kwa sababu kulikuwa na imani kwamba Hamas hawakuwa na nia ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya Israel na kwamba Hamas ilikuwa na nia zaidi ya kusimamia Ghaza.

Shambulio la kihistoria na la kushtukiza la HAMAS lililofanyika Oktoba 7, 2023, limeifedhehesha Israel hasa mashirika yake ya kijasusi ambayo huko nyuma yalikuwa yakijigamba kuwa hayashindiki na eti yana mkono mrefu. 

Mkuu wa vikosi vya jeshi la Israel, Luteni Jenerali Herzi Halevi na mkuu wa shirika la ujasusi la ndani Shin Bet, Ronen Bar wote walikubali kuwajibika baada ya shambulio hilo, lakini wote wanashiriki kwenye vita vya kikatili dhidi ya watu wa Ghaza. 

Anayeonekana ni king'ang'anizi mkubwa wa madaraka ni waziri mkuu wa Isrel, Benjamin Netanyahu ambaye hadi hivi sasa sasa hajakubali kuwajibika, ingawa tafiti zinaonyesha Waisraeli wengi wanamlaumu kwa kushindwa kuzuia au kuulinda utawala wa Kizayuni mbele ya shambulio hilo la HAMAS.