May 06, 2024 02:31 UTC
  • Vyombo vya habari Iraq vimekatazwa kutumia jina 'Israel', vinauita 'Utawala wa Kizayuni'

Vyombo vya habari vya Iraq vimeacha kutumia neno "Israel" kumaanisha utawala wa Tel Aviv na badala yake vinatumia msamiati "Utawala wa Kizayuni" katika hatua ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina kwa miezi kadhaa sasa.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kamisheni ya Vyombo vya Habari na Mawasiliano ya Iraq (CMC).
 
Ali Almuayid amesema katika mkutano na ujumbe wa vyombo vya habari vya Iran mjini Baghdad kwamba kutumia neno 'Israel' kumepigwa marufuku katika vyombo vya habari vya Iraq; na badala yake magazeti na vyombo vya utangazaji vimetakiwa vitumie msamiati 'utawala wa Kizayuni' au 'utawala ghasibu wa Kizayuni'.
 
Almuayid amefichua kuwa, kumekuwepo na shinikizo kutoka Marekani na baadhi ya nchi nyingine kuzuia uamuzi huo, lakini hivi sasa hatua hiyo imetambuliwa rasmi kuwa ni halali kisheria na inatekelezwa nchini Iraq.
 
Mkuu wa Kamisheni ya Vyombo vya Habari na Mawasiliano ya Iraq allitangaza uamuzi huo mara ya kwanza mwezi Januari kutokana na matukio ya Ukanda wa Ghaza na vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo hilo lililowekewa mzingiro, ambavyo hadi sasa vimeshasababisha vifo vya watu wapatao 34,600.

Alisema wakati huo kwamba sheria hiyo pia inaendana na kutimiza wajibu wa kibinadamu, kidini na kimaadili na akaongeza kuwa kutumia neno 'Israel' kunaweza kwa namna fulani kuupa uhalali utawala wa Kizayuni.

 
Mnamo Mei 2022, Bunge la Iraq lilipitisha sheria inayopiga marufuku nchi hiyo kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni na kutangaza rasmi kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai.
 
Katika mkutano huo na ujumbe wa vyombo vya habari vya Iran, Almuayid alisisitiza kuwa ni muhimu sana kuizingatia kadhia ya Palestina na akahimiza kuzidishwa ushirikiano kati ya vyombo vya habari vya Iran na Iraq katika suala hilo.
 
Akiashiria mkutano ujao wa nchi za Kiarabu utakaofanyika katika Muungano wa Falme za Kiarabu, (UAE) Al-Muayad ameelezea mipango na mikakati inayoandaliwa kuutumia mkutano huo kama jukwaa la kampeni kuu ya kutetea haki za Wapalestina.
 
Farshad Mehdipour, Naibu Waziri anayehusika na uenezi wa magazeti na vyombo vya habari katika Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu ya Iran, aliyeongoza ujumbe wa Iran katika ziara ya nchini Iraq, yeye kwa upande wake amependekeza kuandaliwa hafla kubwa nchini Iraq na kuwaalika wanaharakati wa vyombo vya habari wanaounga mkono Palestina na kutumia uwezo wa watu binafsi na maoni ya umma katika nchi zote za Kiislamu kwa ajili ya kulitangaza suala la Palestina.../

 

Tags