May 07, 2024 06:20 UTC
  • Mpira katika uwanja wa Israel kuhusu kusitisha mapigano Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Ismail Haniyah amemfahamisha kuhusu jibu la Hamas kwa pendekezo la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumatatu, Amir-Abdollahian alisema Haniyah anathamini misimamo imara ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Rais Ebrahim Raisi na taifa la Iran katika kuunga mkono Palestina na Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, Haniyah pia alimueleza kuhusu matukio ya hivi punde katika eneo lililoharibiwa na vita la Gaza katika mazungumzo ya simu siku ya Jumapili.

Amesisitiza kuwa, Haniyah amesema amewasilisha jibu la Hamas kwa mpango uliopendekezwa wa pamoja wa Misri na Qatar kuhusu kukomesha mashambulizi ya utawala wa Israel, kubadilishana mateka na kuondoa vikwazo na mzingiro dhidi ya Gaza.

Amir-Abdollahian alimnukuu Haniyah akisema, "Mpira sasa uko kwenye uwanja wa upande wa pili. Hamas ina nia safi."

Taarifa fupi kutoka kwa Hamas siku ya Jumatatu ilisema kuwa harakati hiyo imekubali pendekezo la kusitisha mapigano huko Gaza, ambako imekuwa ikikabiliana na utawala vamizi wa Israel kwa miezi saba.

Hali ya Gaza

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Haniyah aliwafahamisha wapatanishi wa Qatar na Misri kwamba Hamas imekubali pendekezo lao la kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza mapambano au muqawama wa kijasiri wa wananchi wa Palestina mbele ya utawala wa Israel wakati wa vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza katika kipindi cha miezi saba iliyopita.

Jeshi katili la Israel limeua takriban Wapalestina 35,000 huko Gaza tangu tangu lianzishe mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo  Oktoba 7 mwaka jana. Idadi kubwa ya waliouawa ni wanawake na watoto.