Jan 06, 2022 02:52 UTC
  • Rais wa Iraq: Jen. Soleimani alikimbilia kutusaidia katika wakati nyeti

Rais wa Iraq amesema Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), aliitikia mwito wa taifa la Iraq na kwenda haraka kushirikiana na wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu katika wakati hasasi wa kukabiliana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).

Rais Barham Saleh alisema hayo jana Jumatano katika hafla iliyofanyika jijini Baghdad, kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Kamanda Qasem Soleimani, akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashdu Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi vamizi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. 

Rais wa Iraq ameeleza bayana kuwa, "Hii leo tumekusanyika hapa kuwakumbuka viongozi mashujaa ambao walikabiliana na magaidi wa Daesh. Tunauenzi kwa fakhari kubwa ushindi dhidi ya Daesh na namna tulivyofanikiwa kuzima njama zao. Tulipata ushindi dhidi ya Daesh kutokana na fatua ya Mufti Mkuu, Ayatullah Ali al-Sistani."

Kiongozi huyo mkubwa wa Kishia mwaka 2014 alitoa fatua iliyopelekea kuundwa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya Hashdu Sha'abi, ambayo ilikuwa na mchango mkubwa katika vita dhidi ya genge la ISIS.

Mashahidi Soleimani (kushoto) na al-Muhandis

Rais wa Iraq amekumbusha kuwa, "Shahidi Qasem Soleimani, kamanda shupavu wa Iran, pamoja na vikosi na wananchi wa Iraq, walishiriki katika mapambano dhidi ya wananchama wa Daesh, na wakalisaidia taifa letu kuondokana na hatari iliyokuwa imetugubika ya genge hilo la ukufurishaji."

Bahram Saleh amesisitizia haja ya kutafutiwa ufumbuzi changamoto na migogoro inayoshuhudiwa katika eneo la Asia Magharibi, ili kuzuia genge la ISIS na makundi mengine ya kigaidi kuibua fujo na ghasia.

 

Tags