Jun 15, 2023 02:50 UTC
  • Bunge la Lebanon lashindwa tena kumchagua Rais mpya

Bunge la Lebanon hapo jana lilishindwa tena kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo kwa mara ya 12; na kupelekea mkwamo wa kumchagua kiongozi wa juu zaidi nchini humo kuendelea kushuhudiwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, si mgombea anayeugwa mkono na Harakati ya Hizbullah, Suleiman Frangieh wala Waziri wa Fedha wa zamani wa nchi hiyo, Jihad Azour aliyepata kura za kutosha za kumuwezesha kuibuka mshindi katika duru ya kwanza ya upigaji kura

Katika zoezi hilo la jana, Azour aliambulia kura 59, Frangieh akapata kura 51, huku wabunge 18 wakikosa kujaza chochote kwenye makarasati yao ya kupigia kura.

Azour hata hivyo hakutangazwa mshindi kwa kuwa, Bunge la Lebanon lina Wabunge 128 na ili mgombea wa kiti cha urais atangazwe mshindi anapaswa kupata thuluthi mbili ya kura.

Muhula wa urais wa rais wa sasa wa Lebanon Michel Aoun, ulimalizika tangu tarehe 31 Oktoba mwaka jana; na kushindwa kumchagua rais mpya kunashadidisha mgogoro wa ombwe la kisiasa la nchi hiyo kubaki bila ya rais.

Bunge la Lebanon linapaswa kumchagua Rais mpya mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa Rais aliyeko madarakani. Aidha kwa mujibu wa katiba, Rais wa nchi anapaswa kuchaguliwa kutoka miongoni mwa Wakristo wa Kimaroni.

Kutumbukia Lebanon katika mkwamo wa kushindwa kumchagua Rais mpya kunaifanya anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuzidi kuwa tete sambamba na kuongeza matatizo ya kiuchumi ambayo tayari yanaiandama nchi hiyo hivi sasa.

 

Tags