Apr 25, 2024 12:16 UTC
  • Hizbullah: Tumeua na kujeruhi askari 2,000 wa Israel katika operesheni 1,650 tangu vilipoanza vita vya Ghaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imesema imeua na kujeruhi zaidi ya wanajeshi 2,000 wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika operesheni zake 1,650 ilizotekeleza katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala huo katika Ukanda wa Ghaza.

Hizbullah ilitoa takwimu hizo jana Jumatano, kwa mnasaba wa kutimia siku 200 tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha vita vya kikatili na mauaji ya kimbari ambayo hadi sasa yameua idadi kubwa na ya kushangaza ya Wapalestina na kusababisha hali mbaya sana ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza uliouwekea mzingiro.
 
Harakati hiyo ya Muqawama imesema, katika kipindi hicho cha siku 200 imefanya mashambulio 352 ya mizinga, mashambulio 55 ya ndege zisizo na rubani, 727 ya urushaji maroketi ya kutoka ardhini hadi ardhini na makombora 546 yanayoongozwa kwa mitambo pamoja na operesheni 77 za kushambulia kwa bunduki za rashasha kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.
Shambulio la roketi la Muqawama wa Hizbullah

Wapiganaji wa Muqawama wa Lebanon wamesababisha hasara kadhaa kwenye vituo na ngome 344, vifaa vya kiufundi 328, vitengo vya makazi 722, magari ya kijeshi 92, vituo vya kamandi 67, vituo 33 vya mizinga, ndege tano zisizo na rubani, mitambo mitano ya liitwalo Kuba la Chuma, na viwanda viwili vya jeshi la Israel.

 
Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa na Hizbullah ni pamoja na vitongoji 186 vya Waisraeli, maeneo 1,112 yaliyoko kwenye mstari wa mpaka wa pamoja wa Lebanon na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, maeneo 55 ya vituo vya nyuma ya mpaka, na vituo 51 vya angani.
 
Aidha, Hizbullah imebainisha kuwa mashambulizi yake yamewalazimisha walowezi 230,000 wa Kizayuni kuyahama makazi yao kwenye vitongoji 43 vilivyoko kwenye eneo la kilomita tano kutokea mpakani.
 
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Sheikh Naim Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah alitamka bayana kuwa harakati hiyo ya Muqawama haitasitisha makabiliano yake na utawala ghasibu wa Israel na kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza hadi mapigano yatakaposimamishwa.../
 

 

Tags