Kuendelea mgogoro na maandamano ya wananchi nchini Morocco
Katika muendelezo wa machafuko na malalamiko ya wananchi nchini Morocco, askari usalama wa nchi hiyo wamewatia nguvuni makumi ya raia wa nchi hiyo katika mji wa Al Hoceima.
Japokuwa kwa muda sasa maeneo mengi ya Morocco yamekuwa yakisumbuliwa na maandamano na machafuko ya wananchi, lakini hatua hivi karibuni ya serikali ya kumtia mbaroni Nasser Zefzafi, kiongozi wa harakati ya maandamano katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo, imechochea zaidi malalamiko ya wananchi. Zefzafi ambaye anatajwa kuwa mwasisi wa harakati ya wananchi ya 'Al-Harak al-Sha'abi' na kiongozi wa maandamano ya hivi sasa ya kupinga ukosefu wa ajira na ufisadi ndani ya taifa hilo, alitiwa mbaroni hivi karibuni kwa tuhuma za kuvuruga usalama na kufungwa jela katika mji wa Casablanca.
Katika maandamano ya hivi karibuni, maafisa usalama wa mji wa Al Hoceima walitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi katika jaribio la kuuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakionyesha hasira zao kali kutokana na kutiwa nguvuni kiongozi wao. Makumi ya waandamanaji wamejeruhiwa katika maandamano hayo. Mji wa Al Hoceima ulio kaskazini mwa Morocco, ni kitovu cha harakati za upinzani dhidi ya serikali. Tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka 2016, maeneo mengi ya nchi hiyo yalikumbwa na maandamano ya wananchi kufuatia kifo cha muuza samaki kwa jina la Mouhcine Fikri ambaye alipoteza maisha kwa kubinywabinywa ndani ya lori la kuzoa takataka wakati akijaribu kuchukua samaki wake waliotupwa humo na polisi. Licha ya kupita miezi kadhaa tangu kulipojiri tukio hilo, bado mji huo umeendelea kushuhudia maandamano na mikusanyiko dhidi ya serikali.
Waandamanaji wa mji huo wa Al Hoceima wanaamini kwamba, mji huo umetengwa na kupuuzwa na viongozi wa serikali ya Rabat kiasi cha kuufanya ubakie nyuma kimaendeleo. Sambamba na kukosoa kile wanachosema kuwa ni kutozingatiwa matatizo ya mji huo, wametaka kutekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuimarisha miundombinu ya maisha mjini hapo. Awali serikali ya Morocco ilitumia siasa za vitisho na ukandamizaji kwa kutumia kisingizo cha kukabiliana na fikra za kutaka kujitenga kwa eneo hilo.
Sambamba na kuongezeka kwa wimbi la machafuko na kadhalika kupanuka machafuko hayo na kuingia katika miji mingine ya Morocco ukiwemo Rabat, mji mkuu wa nchi hiyo, hivi sasa waandamanaji, mbali na matakwa ya kieneo, wanalalamikia pia ufisadi wa baadhi ya viongozi wa serikali, wanasiasa, makundi ya mamafia na kile wanachokisema kuwa ni ukandamizaji wa serikali na vyombo vya usalama.
Mgogoro wa sasa unajiri katika hali ambayo kwa muda mrefu sasa Morocco inakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kiuchumi likiwemo tatizo la ongezeko la ukosefu wa ajira kwa vijana, ongezeko la madeni ya ndani na nje, ongezeko la upinzani wa ndani na kadhalika tishio la ugaidi. Kabla ya hapo viongozi wa nchi hiyo walitoa ahadi ya kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kuzifanyia mabadiliko sheria kadhaa kwa ajili ya kutatua matatizo ya ndani ya wananchi, lakini pamoja na hayo hawakuweza kufikia lengo hilo.
Wakati huu ambapo wanaharakati wa Morocco wametangaza azma ya kudumisha maandamano yao ambayo kimsingi hayana kifani tangu baada ya yale ya mwaka 2011 katika nchi za Kiarabu hadi watakapopata ushindi, inaonekana kuwa njia pekee inayoweza kuwasaidia viongozi wa nchi hiyo na kuhitimisha mgogoro wa sasa, ni kutekeleza matakwa ya wananchi, ikiwemo kupambana na ufisadi na dhulma, kufanyia marekebisho ya sheria na kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa.