Ushiriki wa Ulaya kwa ajili ya kuwarejesha makwao wahajiri wa Kiafrika
Kuendelea hali mbaya na mazingira mabovu waliyonayo wahajiri huko nchini Libya, kumeufanya Umoja wa Ulaya utangaze azma yake ya kushirikiana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwarejesha katika nchi zao wahajiri hususan wale walioko katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, umoja huo utashirikiana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika kuwarejesha katika nchi zao wahajiri elfu kumi katika miezi michache ijayo.
Matamshi ya Mogherini na ahadi ya Umoja wa Ulaya ya kusaidia kuwarejesha makwao wahajiri wa Kiafrika kutoka Libya vinatolewa katika hali ambayo kumepita zaidi ya mwezi mmoja tangu kufichuliwa kashfa mbaya ya kuweko biashara chafu ya utumwa ambapo wahajiri wa Kiafrika nchini Libya wamekuwa wakiuzwa na kununuliwa kama bidhaa.
Kuendelea kushuhudiwa mgogoro wa kisiasa nchini Libya na kutokuweko serikali kuu yenye nguvu na wakati huo huo kuwa karibu nchi hiyo na Bahari ya Mediterenia ni mambo ambayo yamewafanya wahajiri wa Kiafrika kuichagua nchi hiyo na kuifanya kuwa kivuko chao kizuri kwa ajili ya kuelekea barani Ulaya.
Kwa muktadha huo, akthari ya Waafrika katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni wakiwa na lengo la kuhajiri na kuelekea Ulaya kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri wamekuwa wakituumia njia ngumu na yenye hatari nyingi ya kupitia Libya.
Umasikini, ukosefu wa ajira, vita vya ndani, ugaidi na ukosefu wa amani unaosababishwa na uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya nchi za Kiafrika ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wahajiri wa Kiafrika kuzihama nchi zao na kukimbilia barani Ulaya. Hii ni katika hali ambayo, nchi za Ulaya pia, nazo hususan katika miaka ya hivi karibuni, zinakabiliwa na mgogoro wa wahajiri halali na haramu na viongozi wa nchi hizo wamefanya juhudi za kufunga njia ya wahajiri hao kwa mbinu na mikakati mbalimbali. Kufunga mipaka, kuwapatia makazi wahajiri katika kambi maalumu na kuwatimua wengi kati yao ni miongoni mwa sera za nchi za Ulaya zilizotekelezwa dhidi ya wahajiri. Aidha nchi za Ulaya zikiwa na lengo la kudhibiti wahajiri kuingia katika nchi zao, zinahimiza kuwapatia makazi wahajiri hao nje ya mipaka ya nchi hizo.
Rais Alpha Condé wa Guinea Conakry ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU) anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Kidole cha lawama kinapaswa kuelekezwa kwa nchi za Ulaya. Kwani Umoja wa Ulaya umekuwa ukiunga mkono maafa ya kibinadamu kupitia siasa zake zilizo dhidi ya wahajiri huko nchini Libya.
Ripoti zinaonyesha kuwa, hali ya wahajiri huko nchini Libya ni mbaya mno. Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa, utashirikiana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwarejesha wahajiri wa Kiafrika kutoka Libya katika hali ambayo, utatuzi wa matatizo ya wahajiri hao sio kuwarejesha katika nchi zao bali ni kuyapatia ufumbuzi matatizo yao ya kimaisha na kuboresha maisha yao katika nchi zao. Akthari ya nchi za Kiafrika kipindi fulani zilikoloniwa na madola ya Magharibi hususan Ufaransa na uingiliaji wa madola hayo katika masuala ya ndani ya nchi za Kiafrika daima umekuwa kikwazo cha amani na utulivu wa nchi hizo na kukwamisha mwenendo wa kuboresha uchumi barani Afrika.
Pier Ferdinando Casini, Mkuu wa Kamisheni ya Kigeni na Uhajiri ya Baraza la Seneti la Italia anasema: Ulaya imekuwa ikiwahutubu wahajiri na kupiga nara kwamba, rejeeni makwenu na sisi tutakusaidieni mkiwa katika nchi zenu hizo, lakini huo ni urongo mtupu.