Ung'ang'anizi wa Marekani wa kuendelea kuweko wanajeshi wake nchini Iraq
Msemaji wa komandi ya operesheni za kijeshi ya Marekani huko magharibi mwa Iraq amedai kuwa bado kuna udharura wa kuweko wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo hilo.
Msemaji huyo ametoa visingizio kadhaa vya kudanganya walimwengu na kusema: Licha ya kupita miaka 15 tangu zilipoanza operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iraq, lakini bado hali haijatuliwa hivyo kuna udharura wa kuendelea kuweko wanajeshi wa nchi hiyo nchini humo.
Hivi karibuni televisheni ya al Mayadeen iliripoti kuwa: Wanajeshi wa Marekani wamewataka viongozi wa Iraq kuwatengea maeneo 20 ya kujenga kambi zao za kijeshi. Hayo yamejiri katika hali ambayo viongozi wa Iraq wanapinga kuweko mwanajeshi yoyote wa kigeni katika ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo Marekani inaendelea kushikilia msimamo wake wa kufikiwa maafikiano ya kuendelea kuweko wanajeshi wake nchini Iraq. Duru za kisiasa za Iraq zimesema kuwa, lengo la muda mrefu la Marekani ni kulidhoofisha jeshi la Iraq. Wachambuzi wa mambo wa hata Marekani kwenyewe wanasema kuwa, kuweko wanajeshi wa Marekani katika nchi za Mashariki ya Kati ndiyo sababu ya kuendelea mauaji na vita katika eneo hilo. Scott Bennett mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema kuwa, Marekani imeivamia Iraq bila ya ridhaa ya wananchi wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kuweko wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ni kinyume cha sheria kikamilifu na ni dhihirisho la wazi la jinai za kivita.
Licha ya Wairaq wote kupinga uvamizi wa Marekani na hata bunge la nchi hiyo kupasisha muswada wa kutaka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini mwao lakini Washington inaendelea kuwadanyanga walimwengu kwa kujifanya inaendesha vita dhidi ya ugaidi ili kuhalalisha uvamizi wake katika nchi hiyo ya Kiarabu. Baada ya kutangazwa kusambaratishwa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko Iraq, Wairaq wote bila ya kujali misimamo yao ya kisiasa na kikaumu na kikabila, walisisitiza kuwa, hakuna tena kisingizio cha Marekani kuendelea kubakisha wanajeshi wake nchini humo.
Kwa kweli sisitizo la Marekani la kuendelea kuweko wanajeshi wake nchini humo linaashiria hatari ya kuzuka mgogoro mpya wa kiusalama nchini humo. Wanaotoa tahadhari hiyo wanasema kuwa, hatari iliyopo hivi sasa ni Marekani kuunga mkono baadhi ya makundi ya kisiasa nchini Iraq baada ya kusambaratishwa magaidi wa Daesh na kufanya njma za kuvidhoofisha vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo ili kueneza ubeberu wake kisiasa na kiusalama. Uharibifu mkubwa uliofanywa na magaidi wa Daesh ambao viongozi wenyewe wa Marekani wamekuwa wakitangaza hadharani kuwa ni wao waliowaleta magaidi hao, ni silaha nyingine inayotumiwa na mabeberu hasa Marekani kuendeleza ubeberu wao huko Iraq. Muungano wa kijeshi ulioundwa na Marekani kwa madai ya kupambana na ugaidi nchini Iraq ni mkamilishaji wa ajenda za kuufanya mgogoro wa Iraq kuwa mrefu zaidi. Hii ni katika hali ambayo kwa kufanikiwa kwake kuwasambaratisha na kuwafurusha magaidi wa Daesh, taifa la Iraq limethibitisha kivitendo kuwa linao uwezo wa kulinda usalama wake na kusimamia mambo yake bila ya uingiliaji wa madola ya kibeberu. Hata hivyo mabeberu kwa uongozi wa Marekani wanaonesha wazi kuwa hawako tayari kuiachia vivi hivi Iraq bila ya kuingilia mambo yake ya ndani. Sisitizo la Wamarekani la kuendelea kubakia kijeshi nchini humo kwa njia mbalimbali zikiwemo za kufungua kambi zaidi za kijeshi na pia kufungua njia ya kuingia wanajeshi wa muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi NATO nchini humo, ni miongoni mwa njama zilizoshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni zenye nia ya kuendeleza ubeberu wa madola hayo nchini Iraq.