Jul 21, 2023 07:51 UTC
  • Hizbullah yataka nchi za Waislamu ziwafukuze mabalozi wa Sweden

Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu kuwafukuza mabalozi wa Sweden katika nchi hizo, kulalamikia kitendo cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu katika nchi hiyo ya Ulaya. Hii ni baada ya mkimbizi wa Iraq aliyeko Sweden kuivunjia heshima Qurani Tukufu kwa kuikanyaga na kuipiga mateke mjini Stockholm jana Alkhamisi.

Tovuti ya habari ya al-Ahed imemnukuu Sayyid Hassan Nasrullah, Karibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon akitoa mwito huo katika hotuba aliyoitoa jana Alkhamisi ambapo alieleza kuwa, "Tulichokishuhudia kinalenga kuumiza hisia za Waislamu, na ni wazi aliyeivunjia heshima Qurani Tukufu alipata idhini kutoka serikali ya Sweden, na ni mtu yule yule aliyechoma moto nakala ya Qurani hivi karibuni."

Amewataka Waislamu kote duniani kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya Swala ya Ijumaa hii leo, na kisha kukusanyika nje ya Misikiti huku wakiikumbatia Qurani, ishara ya kukienzi na kukitukuza Kitabu chao hicho kitukufu.

Sayyid Nasrullah amesema kuvunjiwa heshima kwa makusudi Qur'ani Tukufu huko Sweden na katika baadhi ya nchi za Magharibi chini ya usimamizi wa serikali za nchi hizo kunaonyesha kiwango kikubwa cha dhulma na uchokozi dhidi ya Waislamu ambao hawakubali kupotoshwa na upotofu na fikra za Kimagharibi.

Amesema Waislamu kote duniani hasa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu wanapasa kuchukua msimamo thabiti na wa umoja wa kuunga mkono Qurani Tukufu, Maandiko Matakatifu ya Waislamu. 

Serikali ya Iraq tayari imemfukuza balozi wa Sweden mjini Baghdad kulalamikia serikali ya nchi hiyo ya Ulaya Magharibi ya kuruhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Aidha Waislamu katika mitandano ya kijamii wameendeleza kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na Sweden, kulalamikia kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini humo. Baadhi yao wametaka kukatwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na Uswidi kulalamikia uafriti huo.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amelaani vikali hatua ya serikali ya Uswidi ya kuwaruhusu watu wenye misimamo mikali kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu. Hissein Brahim Taha amesitiza kuwa, vitendo hivyo vya kuvunjia heshima matukufu ya kidini ni kielelezo cha kutoheshimu maadili ya kijamii. 

Kadhalika baadhi ya serikali za nchi za Waislamu kama Iran, Uturuki, Qatar, na Saudi Arabia pia zimepinga dharau na utovu wa adabu uliofanyika huko Sweden dhidi ya Quran Tukufu, na kukabidhi malalamiko yao rasmi kwa mabalozi wa nchi hiyo katika nchi zao.

Tags