Wapaestina wakasirishwa na kufufuliwa uhusiano wa Israel na Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10132-wapaestina_wakasirishwa_na_kufufuliwa_uhusiano_wa_israel_na_uturuki
Wananchi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel wameghadhabishwa na hatua ya Uturuki kuhuisha uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala huo, baada ya kuukatiza zaidi ya miaka mitano iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2016 02:49 UTC
  • Wapaestina wakasirishwa na kufufuliwa uhusiano wa Israel na Uturuki

Wananchi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel wameghadhabishwa na hatua ya Uturuki kuhuisha uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala huo, baada ya kuukatiza zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limemnukuu ofisa mmoja mwandamizi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambaye amemkosoa vikali Rais Reccep Teyyip Erdogan wa Uturuki kwa kukubali kibubusa kufufua uhusiano wa Ankara na Tel Aviv. Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema Erdogan ametumia kadhia ya Ukanda wa Gaza kama wenzo wa kisiasa na kusisitiza kuwa matokeo yake yatakuwa mabaya. Haya yanajiri siku mbili baada ya familia za wahanga wa mauaji hayo kukosoa hatua ya kufufuliwa uhusiano wa Ankara na Tel Aviv. Jana Jumatatu, Uturuki na Israel zilitangaza rasmi kufufua uhusiano wa pande mbili.

Uhusiano wa Ankara na Tel Aviv uliingia doa baada ya jeshi la majini la utawala ghasibu wa Israel kuwaua kwa kuwamiminia risasi wanaharakati wa Uturuki mwaka 2010. Kwenye uvamizi huo, makomandoo wa Israel waliwaua wanaharakati 9 raia wa Uturuki na kujeruhi wengine 50, wakati meli yao ilipokuwa katika maji ya kimataifa katika Bahari ya Mediterranean ikipeleka misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza mnamo Mei 31 mwaka 2010. Kufutia tukio hilo na hatua ya Israel kukataa kuomba radhi kutokana na kitendo chake hicho cha kichokozi, Uturuki ilikata uhusiano wake wa kijeshi na Tel Aviv na kumtimua balozi wa utawala huo ghasibu mjini Ankara sambamba na kumuita nyumbani balozi wake, Septemba mwaka huo.