Kata'ib Hizbullah: Tutasambaratisha 'miradi ya US' Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101424-kata'ib_hizbullah_tutasambaratisha_'miradi_ya_us'_asia_magharibi
Harakati ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imeionya vikali Marekani na kusema kuwa itasambaratisha miradi ya Washington katika eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 24, 2023 07:32 UTC
  • Kata'ib Hizbullah: Tutasambaratisha 'miradi ya US' Asia Magharibi

Harakati ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imeionya vikali Marekani na kusema kuwa itasambaratisha miradi ya Washington katika eneo la Asia Magharibi.

Taarifa ya harakati hiyo ambayo ni sehemu ya muungano wa vikosi vinavyopambana na ugaidi nchini Iraq vya Hashdu Shaabi ilitoa indhari hiyo jana Jumatano na kusisitiza kuwa, wapambanaji wake watakabiliana na njama za Marekani katika eneo hili.

Harakati hiyo ya muqawama ya Iraq imeeleza kuwa, harakati na mienendo ya misafara ya kijeshi ya Marekani katika baadhi ya miji ya Iraq hivi karibuni ni ushahidi tosha kuwa maadui wana azma ya kubakisha vikosi vyake katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Washington ina wanajeshi zaidi ya 2,500 ndani ya ardhi ya Iraq, licha ya Bunge la nchi hiyo ya Kiarabu kupasisha azimio la kutaka kuondoka wanajeshi hao vamizi.

Azimio hilo lilipasishwa Januari 2020, baada ya jeshi la kigaidi la US kuwaua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na naibu mkuu wa zamani wa Hashdu Shaabi, Abu Mahdi al-Muhandis.

Vikosi vinavyopambana na ugaidi nchini Iraq vya Hashdu Shaabi

Harakati ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya wanajeshi wa Marekani walioko nchini humo yataendelea hadi wanajeshi wote wa nchi hiyo watakapoondoka katika ardhi ya Iraq. Imesema mapambano dhidi ya wavamizi ni haki ya kisheria ya watu wa Iraq na lengo lake ni kuwalazimisha askari vamizi kuondoka katika ardhi ya Iraq

Aghalabu ya wananchi wa Iraq wanataka vikosi vya wanajeshi vamizi wa Marekani viondoke katika ardhi ya nchi hiyo hususan baada ya Bunge la Taifa la nchi hiyo kutoa agizo likitaka kuondoka wanajeshi wote vamizi nchini Iraq.