Jun 30, 2016 03:32 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya kigaidi Istanbul, Uturuki

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya kigaidi dhidi ya uwanja wa ndege mjini Istambul nchini Uturuki, yaliyosababisha vifo vya makumi ya watu na wengine wengi kujeruhiwa.

Bahram Qassemi, msemaji wa Wizaya ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amelaani hujuma hiyo ya kigaidi dhidi ya uwanja wa kimataifa wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul, usiku wa kuamkia jana, ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa hujuma hiyo, msemaji wa Wizaya ya Mashauri ya Kigeni wa Iran ametaja mashambulizi hayo kuwa jinai isiyo ya utu. Wakati huo huo, Hassan Qashqavi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amethibitisha kuwa Muirani mmoja ameuawa katika mashambulizi hayo na wengine watano kujeruhiwa.

Hapo jana Ban Ki -moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa taarifa na kulaani mashambulizi ya kigaidi ya Jumanne usiku katika uwanja wa ndege wa Istanbul na kutaka kuwepo ushirikiano mkubwa wa kimataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Watu waliokuwa na mada za miripuko Jumanne usiku waliingia katika uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul na kuripua mada hizo katika maeneo matatu ya uwanja huo. Duru za habari zimearifu idadi ya watu waliopoteza maisha katika mashambulizi hayo ya kigaidi kuwa ni 41 na zaidi ya 140 wamejeruhiwa.

Tags