Syria: Damu ya Mashahidi itaongeza azma yetu ya kupata ushindi kamili
(last modified Fri, 06 Oct 2023 11:10:24 GMT )
Oct 06, 2023 11:10 UTC
  • Syria: Damu ya Mashahidi itaongeza azma yetu ya kupata ushindi kamili

Ofisi ya Rais wa Syria imetoa taarifa ikizungumzia kushindwa ugaidi mbele ya irada na uwezo wa nchi hiyo na kusisitiza kwamba damu ya Mashahidi wa chuo cha kijeshi cha Homs inaongeza azma ya Damascus ya kufikia ushindi kamili.

Ilikuwa jana alasiri (Alhamisi, Oktoba 5) ambapo televisheni rasmi ya Syria ilitangaza shambulio la ndege zisizo na rubani lililolenga mahafali ya wahitimu wa chuo cha kijeshi katika mkoa wa Homs na kuripoti  kuwa shambulio hilo limesababisha maafa makubwa ya roho za watu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la SANA, ofisi ya rais wa Syria leo imetoa taarifa kuhusu jina hiyo ya kigaidi na kusisitiza juu ya azma ya Damascus ya kuendeleza mapambano dhidi ya ugaidi hadi kufikia ushindi kamili.

Taarifa ya ofisi ya rais wa Syria imesema: "usaliti, jinai na ugaidi vimetoa pigo la kuwadhuru watu wa nchi hii na kuzigeuza nyakati za furaha na fahari kuwa za huzuni na machungu".

Ofisi ya Rais wa Syria imesisitiza kwamba: "ugaidi hauwezi kamwe kudhoofisha nguvu zetu, kuturejesha nyuma katika uthabiti wetu na kuitia shaka imani yetu".

Eneo lililolengwa na shambulio la kigaidi la droni

Taarifa hiyo ya serikali ya Damascus imeendelea kubainisha kuwa: "kila tone la damu lililodondoka chini hapo jana katika Chuo cha Kijeshi cha Homs litaongeza nguvu, mshikamano na azma yetu ya kukamilisha ushindi".

Kufuatia tukio hilo, Wizara ya Afya ya Syria imetangaza leo asubuhi kwamba, idadi ya Mashahidi wa shambulio la kigaidi la Homs imeongezeka na kufikia 89, wakiwemo wanawake 31 na watoto 5; na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 277.
Taarifa ya serikali ya Damascus imeutaka pia Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama zilaani shambulio la makundi ya kigaidi katika chuo cha kijeshi cha nchi hiyo huko mkoani Homs.


Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetoa taarifa na kulaani vikali jinai ya makundi ya kigaidi huko Homs, ambapo mbali na kuitaja hatua magaidi hao kuwa ni kitendo cha woga, imetaka nchi zinazounga mkono ugaidi zikemewe.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimetoa taarifa za kulaani jinai iliyofanywa hapo jana na magaidi katika mahafali ya wahitimu wa chuo cha kijeshi cha Syria katika mkoa wa Homs.../