Kukaribisha HAMAS azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekaribisha azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza na kutangaza kuwa inataka Baraza Kuu la umoja huo na taasisi zingine husika za kimataifa kutekeleza hatua za lazima kwa ajili ya utekelezaji wa haraka wa azimio hilo ili vivuko vya Gaza vifunguliea tena na hivyo kuruhusu nishati ya mafuta na misaada ya haraka ya kibinadamu iwafikie watu wa eneo hilo.
Viongozi wa Hamas na Mamlaka ya Ndani ya Palestina wamekaribisha azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kutaka litekelezwe mara moja.
Baada ya kupita wiki tatu tangu kuanza hujuma za Israel dhidi ya Gaza, hatimaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa lilipiga kura na kupitisha azimio la kulinda raia wakati huu ambapo utawala haramu wa Israel umeshadidisha hujuma dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Azimio hilo limepitishwa katika kikao cha 10 cha dharura ambacho kilifanyika Ijumaa kwa siku ya pili huku kukiwa na mvutano kwenye Baraza la Usalama na hali katika eneo linalozingirwa la Gaza ikizidi kuwa mbaya.
Azimio hilo linataka suluhisho la haraka, la kudumu na endelevu la kibinadamu. Azimio hilo ambalo lilipendekezwa na Jordan limepitishwa na Baraza Kuu, kwa kura 120 za ndio, 14 za hapana na nchi 45 zimejuzuia kupiga kura.
Katika Baraza Kuu nchi wanachama 193 kila moja ina kura moja, na tofauti na Baraza la Usalama, hakuna kura ya turufu. Maamuzi ya Baraza Kuu kuhusu masuala muhimu hufanywa na theluthi mbili ya wajumbe walihudhuria kikao na kupiga kura. Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiendesha vita dhidi ya Gaza tangu tarehe 7 Oktoba, wakati harakati za muqawama za kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas na Jihadul Islami zilipoanzisha operesheni yao kubwa zaidi kama jibu kwa jinai za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Baraza Kuu pia limesema kuwa linakataa vikali jaribio lolote la kuwahamisha raia wa Palestina kwa nguvu. Azimio hilo la Baraza Kuu limekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa mara nne katika wiki mbili zilizopita kuchukua hatua kutokana na Marekani kupiga kura ya turufu mara kwa mara dhidi ya maazimio dhidi ya Israel.
Kutokuwa na uwezo wa Baraza la Usalama kuidhinisha azimio hilo kulitilia shaka na kuchafua itibari ya Umoja wa Mataifa. Kwa kupitisha azimio hili, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeonyesha kuwa tofauti na Baraza la Usalama, Baraza Kuu ni taasisi ya kisheria, na si ya kisiasa. Wajumbe wengi wa Baraza Kuu wanafadhilisha haki na uadilifu kuliko utashi wa kisiasa na hawako tayari kuwa washirika wa kuua watu wa Gaza.
Kuna nukta kadhaa kuhusiana na hatua ya Hamas ya kukaribisha azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa:
Nukta ya kwanza ni kwamba; Suala la Palestina linaungwa mkono na nchi nyingi duniani, na licha ya njama na mashinikizo ya Marekani na utawala wa Kizayuni, lakini nchi nyingi duniani zinaiunga mkono Palestina na zinaulaani utawala wa Kizayuni.
Pili; Hamas si tu kwamba haijasambaratishwa kutokana na mashambulizi ya kila upande ya utawala wa Kizayuni, bali bado ni moja ya makundi mahiri na muhimu ya muqawama ambayo yana uungaji mkono wa wananchi na yapo katika medani.
Tatu, katika kivuli cha kigugumizi na utepetevu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuhusiana na matukio ya Gaza, Harakati ya Hamas inakaribisha juhudi za kimataifa za kukomesha vita na kutuma misaada ya kibinadamu, na wakati huo huo, ina utayari wa lazima wa kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, ikiwa ni pamoja na vita vya ardhini.
Nne ni kwamba; Hamas inafahamu vyema hali ya kisiasa na utendakazi usio wa haki wa Baraza la Usalama. Madola ya Magharibi ambayo daima yamekuwa yakidai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu, hivi sasa ni washirika wa jinai za utawala wa Kizayuni na yamefumbia macho hata kuuawa shahidi takriban watoto 3,000 wa Kipalestina na wanawake 1,500 kutokana na mashambulizi ya utawala huo ghasibu wa Kizayuni.
Kwa hivyo, inapasa kusema kuwa, kukaribishwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni kejeli kwa utendaji kazi wa Baraza la Usalama kuhusu jinai za kivita za utawala wa Kizayuni.