Bahrain yasitisha uhusiano wa kibiashara na Israel, yamrejesha nyumbani balozi wake
Bunge la Bahrain limetangaza kuwa, limesitisha uhusiano wa kiuchumi na utawaa wa Kizayuni wa Israel na kuwaondoa mabalozi wake kutokana na kuendelea mashambulio ya jeshi la Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Naibu wa Kwanza wa Spika wa Bunge, Abdel-Nabi Salman, amethibitisha uamuzi huo kwa shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa "mzozo unaoendelea Gaza hauwezi kunyamaziwa ukimya."
Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa, bado uamuzi huo wa Bunge haujathibitishwa na serikali ya Manama. Ikiwa uamuzi huo utathibitishwa na serikali, hii itakuwa hatua ya kwanza kuchukuliwa na mmoja wa washirika wa Kiarabu wa Israel katika Ghuba ya Uajemi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, Wabunge wa Bahrain wakilalamikia jinai za Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel wamemuita nyumbani balozi wa nchi hiyo aliyeko Tel Aviv.
Bahrain ni mmoja washirika wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo imekuwa ikishuhudia maandamano ya kulaani jinai za Israel.
Ikumbukwe kuwa, Septemba 2020, viongozi wa Bahrain na wa utawala haramu wa Israel walisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mbele ya rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.
Kufuatia kusainiwa makubaliano hayo ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Bahrain na utawala haramu wa Israel, wananchi wa Bahrain mara kwa mara wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga uhusiano huo.
Sambamba na hayo, utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain umeendelea kuandamwa na uukosoaji mkkubwa kutokana na kuuruhusu utawala haramu wa Israel kufungua ubalozi wake katika nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi.