Sisitizo la Uturuki la kuendelea kuwepo kijeshi nchini Iraq na Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104594-sisitizo_la_uturuki_la_kuendelea_kuwepo_kijeshi_nchini_iraq_na_syria
Mashambulizi ya jeshi la Uturuki dhidi ya Syria na Iraq yamewekwa katika ajenda ya serikali ya Ankara, muda mfupi baada ya Anthony Blinken Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kufanya safari mjini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2023 04:24 UTC
  • Sisitizo la Uturuki la kuendelea kuwepo kijeshi nchini Iraq na Syria

Mashambulizi ya jeshi la Uturuki dhidi ya Syria na Iraq yamewekwa katika ajenda ya serikali ya Ankara, muda mfupi baada ya Anthony Blinken Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kufanya safari mjini humo.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kwamba mashambulizi ya anga ya jeshi dhidi ya makundi ya kigaidi kaskazini mwa Iraq na Syria yataendelea. Amesema Uturuki itawalenga magaidi kwa ndege za kivita, makombora na ikibidi kupitia mashambulizi ya nchi kavu. Erdogan pia amesisitiza kuwa operesheni za anga za Uturuki nchini Syria na Iraq zitaongezeka kwa lengo la kuwaangamiza magaidi popote pale watakapokuwa.

Kushambuliwa wanamgambo wa chama cha Kurdistan cha Uturuki PKK katika ardhi za Syria na Iraq siku moja  baada ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mjini Ankara ni jambo la kuzingatiwa. Katika safari yake katika nchi kadhaa za eneo, Blinken kimsingi alibadilishana mawazo na viongozi wa nchi kama vile Jordan, Misri na India kuhusiana na masuala ya Ukanda wa Gaza. Hii ni katika hali ambayo, akiwa mjini Ankara, alijadiliana na viongozi wa Uturuki masuala ya pembeni kama vile kufunguliwa njia ya kupitishwa nafaka na masuala ya Ukraine pamoja na uanachama wa Uswiss katika Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO.

Wanajeshi wa Uturuki

Mbali na hayo, Blinken pia amewabainishia viongozi wa Ankara siasa za Marekani kuhusiana na masuala ya Ukanda wa Gaza na kuwapa maelekezo katika uwanja huo. Muamala wa aina hiyo wa kiongozi wa ngazi za juu wa Marekani na viongozi wa Uturuki unaonyesha kuwa Washingtone imeiondoa nchi hiyo katika orodha ya waitifaki wake wa Asia Magharibi. Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Washington bado wanaendeleza siasa zao za kuingilia na kuwaainishia viongozi wa Ankara mambo wanayopasa kufanya kuhusu siasa zao za ndani na nje.

Ni dhahiri kwamba mvutano kati ya Uturuki na Syria na vilevile Iraq utakuwa kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. Kwa sababu hiyo, hatupaswi kupuuza dhana kwamba huenda Marekani imeiamuru Uturuki kuzidisha mgogoro wake na nchi za Syria na Iraq ili kwa njia hiyo iweze kupunguza wasiwasi wa mshirika wake haramu katika eneo, yaani utawala wa Kizayuni. Huenda viongozi wa Ankara wanajaribu kuanzisha mashambulizi mapya huko Syria na Iraq ili kuwashinikiza viongozi wa White House wajibu matakwa yao. Hii ni katika hali ambayo, nchi za Magharibi na haswa Marekani zina ushawishi mkubwa katika miundo ya kisiasa, kijeshi, kiidara na hata kiuchumi ya Uturuki. Ni kutokana na ukweli huo ndipo, wataalamu wengi wa Magharibi na hata viongozi wa White House wakasema kuwa gurudumu la mfumo wa uchumi wa Uturuki liko mikononi mwa Marekani.

Ikiwa mwanachama hai wa Jumuiya ya Kujihami NATO, Uturuki ilitarajia kwamba washirika wake wangeisaidia kijeshi wakati wa kuvamia na kuteka ardhi za Syria na Iraq. Serikali ya Uturuki iliteka sehemu ya ardhi ya Syria mnamo 2018, wakati Marekani na washirika wake walituma vikosi vyao vya kijeshi nchini humo. Kuhusiana na hayo, gazeti la Yeni Shafaq linalofungamana na serikali ya Ankara hivi karibuni lilichapisha makala iliyofichua kuanzishwa na kuundwa kwa kundi la kigaidi la kitakfiri la Daesh na Marekani na kukiri kuwa: Vita vya kijeshi nchini Syria vimethibitisha ukweli kwamba Marekani si nchi ya kuaminika. Kwa sababu inaunga mkono makundi ya kigaidi na kuwatumia watoto kufanya operesheni za kujilipua kwa mabomu na kijeshi katika maeneo tofauti ya Iraq na Syria.

Jeshi la Uturuki nchini Syria

Kwa upande mwingine, Bunge la Uturuki hivi karibuni liliongeza karibu mara mbili bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo kwa ajili ya mwaka ujao wa 2024 na kusema, mojawapo ya sababu za kuongezwa bajeti hiyo ni kuendeleza operesheni za kijeshi nchini Syria na Iraq. Hatua hiyo ya wabunge wa nchi hiyo inaonyesha kuwa siasa za serikali ya Uturuki zimejikita katika kukabiliana na kuwakandamiza wanamgambo wa Kikurdi wa Uturuki na Syria wa Chama  cha PKK. Awali, viongozi wa serikali ya Erdogan walikitangaza chama hicho kuwa ni chama cha wanaotaka kujitenga na kukijumuisha katika orodha ya makundi ya kigaidi. Aidha tangu mwaka 2018, serikali ya Uturuki imekuwa ikitumia kidingizio cha kupambana na chama  cha Kikurdi cha PKK, kulenga maeneo ya kaskazini mwa Syria na Iraq.

Kwa mukhtasari tunaweza kusema kuwa, jibu la kwanza la serikali ya Uturuki kwa takwa la Marekani, siku moja baada ya kufanyika safari ya waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo mjini Ankara, ni kushambuliwa kijeshi makundi ya Kikurdi ambayo yako chini ya himaya na uungaji mkono maalumu wa Marekani.