Siku 37 za vita vya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104734-siku_37_za_vita_vya_gaza
Jumapili vita vya Ghaza viliingia katika siku ya 37 , huku utawala wa Kizayuni ukiendeleza mashambulizi na jinai zake za kinyama dhidi ya wakazi wa Gaza na hasa kwa kushambulia kikatili hospitali, shule, kambi za wakimbizi, wahudumu wa afya, wagonjwa na majeruhi kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani.
(last modified 2024-05-29T07:24:47+00:00 )
Nov 13, 2023 22:54 UTC
  • Siku 37 za vita vya Gaza

Jumapili vita vya Ghaza viliingia katika siku ya 37 , huku utawala wa Kizayuni ukiendeleza mashambulizi na jinai zake za kinyama dhidi ya wakazi wa Gaza na hasa kwa kushambulia kikatili hospitali, shule, kambi za wakimbizi, wahudumu wa afya, wagonjwa na majeruhi kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani.

Wanajeshi katili wa Kizayuni wanaendelea kuzingira hospitali za Ghaza, ikiwemo hospital ya al-Shifa, na wanampiga risasi mtu yeyote anayejaribu kuondoka au kuingia katika majengo ya hospitali hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Ukanda wa Ghaza ameeleza kuwa, hospitali ya al-Shifa imekabiliwa na mashambulizi makali zaidi ya anga ya utawala wa Kizayuni, na wanajeshi vamizi wako umbali wa mita 100 kutoka hospitali hiyo ambapo wanamlenga mtu yeyote ambaye anaingia au kutoka hospitalini hapo.

Hospitali nyingine za Gaza zina hali kama hiyohiyo ya Hospitali ya al-Shifa, na Hilali Nyekundu ya Palestina imeripoti kwamba vifaru vya Israel viko umbali wa mita 20 kutoka hospitali ya Al-Quds ambapo wanajeshi wa utawala ghasibu wanawafyatulia risasi za moja kwa moja wakimbizi waliokimbilia usalama wao katika jengo hilo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pia limeonya kwamba maisha ya watoto milioni 1 wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza yako hatarini kutokana na kukaribia kusambaratika kabisa sekta za huduma na afya za eneo hilo.

Huku ikiashiria kuzima mashine za dharura katika hospitali za Al-Nasr na Al-Rentisi ambazo ni maalumu kwa  watoto, UNICEF imetangaza kuwa kuendelea kushambuliwa hospitali hizo kunatishia maisha ya watoto hasa walio na matatizo ya figo (wanaofanyiwa dialysis) na wanahitajia uangalizi maalum. Aidha, maelfu ya watoto kaskazini mwa Gaza wanakabiliwa na hali mbaya sana kutokana na kukosa mahali salama pa kwenda, kuishi chini ya mashambulizi makali na kukosena huduma za kimsingi za maisha.

Hali ya kusikitisha ya hospitali za Gaza

Upasuaji mgumu unaofanyika bila ganzi katika yadi za hospitali tena kwa mwangaza mdogo wa simu, kukatwa maji, umeme na chakula, kurundikana maiti, vifo vinavyoendelea vya watoto wachanga na hata miongoni mwa madaktari ni matukio ambayo Gaza inayashuhudia siku hizi katika kivuli cha mashambulizi ya kinyama na kibaguzi ya Wazayuni makatili.

Idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya kila mara ya utawala huo ghasibu imefikia zaidi ya watu 11,200, ambapo 8,000 ni watoto, wanawake na wazee. Zaidi ya watu 28,000 pia wamejeruhiwa.

Hali inayotawala Gaza inatoa udharura wa kutekelezwa mapendekezo 10 ya Rais wa Iran aliyoyatoa katika mkutano dharura wa viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Kiarabu mjini Riyadh, Saudi Arabia.

Katika kikao cha pamoja cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Nchi za Kiarabu kuhusu suala la Gaza, kilichofanyika Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, rais Seyyed Ebrahim Raisi alitoa mapendekezo 10 ya dharura kwa ajili ya kuwasaidia wananchi madhulumu wa Palestina, ambayo ni: Kukomeshwa mauaji ya watu wa Gaza, kuondolewa kikamilifu mzingiro ambao unatekelezwa kwa miaka mingi na utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, kuondoka mara moja jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo hilo, kukata  nchi za Kiislamu uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na utawala wa Kizayuni, kuanzishwa mahakama ya kimataifa, kuwafungulia mashtaka na kuwaadhibu viongozi wa Kizayuni na Marekani wanaohusika na jinai za kivita huko Gaza, kuanzishwa mfuko maalum wa nchi za Kiislamu kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza na kutumwa msafara wa meli zinazobeba misaada ya kibinadamu kwa watu wa Palestina kutoka nchi za Kiislamu.

Machungu ya wakazi wa Gaza

Wakati huo huo mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya muqawama vya Palestina na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika maeneo tofauti ya mji wa Ghaza. Siku 12 zimepita tangu kuanza operesheni ya nchi kavu ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, na vikosi vya adui vinavyouzunguka bado havijaweza kufika katika maeneo ya makazi ya eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza, ambapo vinapata vipigo vikali kutoka kwa makundi ya muqawama katika sehemu mbalimbali za eneo hilo.

Abu Obeidah, Msemaji wa Brigedi za al-Qassam tawi la kijeshi la harakati ya Hamas  ametangaza kwamba vifaru vya utawala wa Kizayuni vinakabiliwa na mapambano makali ya makundi na vikosi vya kimuqawama ambayo yamevilazimu virejee nyuma na kubadili mwelekeo wao.

Akizungumzia kuharibiwa kabisa vifaru na magari ya kijeshi zaidi ya 160 ya jeshi la Kizayuni katika vita hivyo amesisitiza kuwa: Kujitolea mhanga wanamqawama ni utangulizi wa ushindi.

Kushindwa mapema utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza kunaonyesha kuwa Israel baada ya vita hivyo itakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa.

Viongozi wa Israel walianzisha vita vya Gaza huku wakiwa na uungaji mkono wa asilimia 27 na jeshi pia likiwa na uungaji mkono wa asilimia 51 tu wa Wazayuni. Haya ni pamoja na kuhamishwa Wazayuni 250,000 kutoka maeneo yaliyo karibu na mipaka ya Gaza na kuwepo mateka 240 mikononi mwa makundi ya muqawama.