Umuhimu wa maneno ya Kiongozi wa Ansarullah kuhusu vita vya Gaza
Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Ansurullah ya Yemen ameashiria katika hotuba yake uungaji mkono wa pande zote wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na kukosoa misimamo ya nchi 57 za Kiarabu na Kiislamu kuhusiana na suala muhimu la Ghaza.
Kwanza Abdul Malik al-Houthi amekosoa vikali mkutano wa Saudi Arabia, ambao ulifanyika karibuni katika fremu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inayojumuisha nchi 57 za Kiarabu na Kiislamu kwa kushindwa kuchukua hatua yoyote ya kivitendo juu ya suala hilo muhimu na kutosheka tu kwa kutoa taarifa isiyokuwa na uzito wowote wa maana.
Kuhusiana na hilo, Abdul Malik al-Houthi amesema: Mkutano eti unaowakilisha Waislamu wote umetoa tamko tu bila kuchukua msimamo wa kivitendo wa kuunga mkono Gaza. Je, uwezo na nguvu hiyo ni zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu?
Kutochukua hatua muhimu nchi za Kiarabu na Kiislamu dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni kumeufanya utawala huo kuendeleza mauaji ya kimbari na ya kutokomeza kizazi cha watu wa Ghaza. Utawala huo umefikia natija kwamba hata mauaji ya halaiki ya watu wa Gaza hayataugharimu chochote katika uga wa uhusiano wake na nchi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu. Baadhi ya nchi za Kiarabu ziliwasilisha kwa udhalili ujumbe kwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kwamba hazina tatizo lolote na kuangamizwa Hamas na utawala huo. Abdul Malik al-Houthi ameashiria hayo katika hotuba yake na kusema: Baadhi ya nchi za Kiarabu zinataka Gaza isiongozwe na wapiganaji wa muqawama wa Palestina Hamas na iwe chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa Wazayuni au Mamlaka ya Ndani ya Palestina, asasi ambayo hata haina uwezo wa kudhibiti Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, achilia mbali Gaza.
Huku nchi za Kiarabu na Kiislamu zikichukua misimamo ya kulegalega na dhaifu kuhusiana na jinai za Wazayuni, Wayemen wanaonyesha uungaji mkono wao wa dhati kwa watu wa Gaza kwa njia ya kivitendo. Mashambulio ya makombora ya Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni yamesababisha meli za Israel kupita kinyemela na kwa wasiwasi mkubwa katika lango la Bab al-Mandab na Bahari Nyekundu. Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen amesema katika muktadha huo: Harakati za kimagendo za meli za Kizayuni ndiyo sababu ya hofu yao, utawala ambao bendera yake inapepea katika balozi zake za nchi za Kiarabu lakini hauthubutu kuweka bendera yake kwenye meli zake zinazopita katika Bahari ya Shamu. Sisi hatuna wasiwasi wowote wa kulenga meli hizo.
Wananchi wa Yemen pia wameonyesha upinzani wao dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni kwa kuhudhuria kwa makumi ya maelfu ya watu katika maandamano yanayofanyika katika miji tofauti ya nchi hiyo ukiwemo wa Sana'a na kwa mujibu wa maneno ya Kiongozi wa Ansarullah kama njia za kuingia Gaza zingekuwa wazi basi mamia ya maelfu ya Wayemen wangekuwa tayari kwenda kupigana bega kwa bega na wenzao wa Gaza dhidi ya adui Mzayuni.
Suala jingine ni uungaji mkono wa Marekani kwa Wazayuni katika vita vya Gaza. Huku wakitoa uungaji mkono wa kivitendo kwa Wazayuni, Wamarekani pia wameziwekea mashinikizo nchi za Kiarabu na Kiislamu zijiepushe kuchukua hatua zozote za kivitendo kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Gaza. Abdul Malik al-Houthi amesema: Wamarekani wanatushinikiza ili tusiwaunge mkono wapalestina kwa kututishia kurejea mapigano nchini nchini kwetu na kukwamisha mchakato wa kusitisha kwa vita, lakini watu wetu kamwe hawatasalimu amri mbele ya Marekani, Uingereza na waitifaki wake.