Makundi ya muqawama yatoa mwito wa kufanyika 'mgomo wa ulimwengu'
Muungano wa makundi ya muqawama wa Palestina umetoa mwito wa kufanyika 'mgomo kamili wa kimataifa' kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, ambao wanakabiliwa na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Katika taarifa ya jana Jumamosi, Vikosi vya Kitaifa na Kiislamu, ambao ni mwavuli wa muungano wa makundi makubwa ya muqawama wa Palestina, vilitoa mwito wa kufanyika mgomo wa ulimwengu mzima kesho Jumatatu, kwa lengo la kulaani jinai za kutisha za Israel dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Gaza.
Taarifa hiyo imesema: Tunataraji kuwa ulimwengu mzima utashiriki mgomo huo, ambao unakuja katika muktadha wa harakati kubwa ya kimataifa, itakayojumuisha shakhsia mashuhuri.
Muungano wa makundi ya muqawama wa Palestina umesisitiza kuwa, harakati hiyo ya kimataifa imesisimama kidete dhidi ya mauaji ya kimbari na kuangamizwa kizazi cha Wapalestina, na vile vile dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wakoloni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Shehab, mgomo huo wa kimataifa wa kesho Jumatatu unatazamiwa kuathiri sekta za usafiri na uchukuzi, safari za ndege, biashara, benki, bandari, skuli na hata Vyuo Vikuu vya nchi zitakazoshiriki.
Hii ni katika hali ambayo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) juzi Ijumaa ilizitolea wito nchi za Kiarabu, Kiislamu na wapigania uhuru kote duniani kuendeleza maandamano ya kutangaza mshikamano na kuwa pamoja na wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, Wapalestina zaidi ya 17,700 wameuawa shahidi, mbali na wengine wasiopungua 48,780 kujeruhiwa katika hujuma na mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza tokea Oktoba 7.