Dec 15, 2023 10:38 UTC
  • UN: Nusu ya wakazi wa Gaza katika hatari ya kufa njaa

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, asilimia 50 ya wakazi wa eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu wapo hatari ya kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa.

Carl Skau, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) amesema hayo katika makao makuu ya umoja huo mjini New York na kuongeza kuwa, "Ukweli unaotisha ni kwamba, watu tisa kati ya kila watu kumi (Gaza) hawali vizuri, hawali kila siku na wala hawajui mlo wao ujao utatoka wapi."

Kanali ya Press TV imemnukuu Skau akisema kuwa, WFP ilifanikiwa kusambaza chakula cha msaada katika Ukanda wa Gaza wakati wa usitishaji vita kwa muda wa siku saba, lakini imeshindwa kuendelea na mpango huo baada ya kuanza upya vita katika eneo hilo.

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesisitizia udharura wa kusimamishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo, sambamba na kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililo chini ya mzingiro.

Watoto ndio wahanga wakuu wa jinai za Israel huko Gaza

Skau amebainisha kuwa, iwapo mazingira yataruhusu, shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) litasambaza misaada hiyo kwa Wapalestina wengine milioni moja wa Gaza ndani ya wiki chache.

Mwito huo wa kusimamishwa mapigano Gaza umetolewa katika hali ambayo, Marekani mara kadhaa imelipigia kura ya veto azimio la kusitisha vita Gaza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; kitendo ambacho kimeendelea kulaaniwa kimataifa.

Zaidi ya Wapalestina 18,800 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa shahidi wakati wa vita vya mauaji ya halaiki ambavyo Israel ilivianzisha tarehe 7 Oktoba, kufuatia operesheni iliyofanywa na makundi ya muqawama ya Gaza iliyopewa jina la Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.

Tags