Wizara ya Ulinzi ya Marekani: Hatujaweka ratiba yoyote ya kuondoka Iraq
(last modified Wed, 10 Jan 2024 06:19:49 GMT )
Jan 10, 2024 06:19 UTC
  • Wizara ya Ulinzi ya Marekani: Hatujaweka ratiba yoyote ya kuondoka Iraq

Patrick Ryder, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon amesema, nchi hiyo haina mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake walioko nchini Iraq.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ryder ameyasema hayo katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari huko Pentagon, ambapo sambamba na kulitaja genge la kigaidi la DAESH (ISIS) kama kisingizio cha hatua hiyo inayochukuliwa na Washington, ameongezea kwa kusema, "kwa sasa, hakuna mpango wowote wa kuondoka ambao mimi ninaweza kuwa na taarifa nao. Tunaendelea kujikita katika kuwashinda ISIS".

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, msemaji wa Pentagon amedai kuwa, wanajeshi 2,500 wa Marekani wako nchini Iraq kwa mwito wa serikali ya nchi hiyo, na akaendelea kudai kwamba hana taarifa yoyote kutoka Baghdad iliyotumwa kwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani kuhusu uamuzi wa kuwatimua wanajeshi hao.

Askari wa jeshi vamizi la Marekani waliopiga kambi Iraq

Ryder anadai hayo wakati serikali ya Iraq ilitangaza wiki iliyopita kwamba inapanga kuanza kutekeleza mchakato wa kuufukuza katika ardhi ya nchi hiyo muungano wa kimataifa wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.

Hapo awali na katika mjibizo aliotoa kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa mamlaka ya kujitawala ya Iraq unaofanywa na muungano wa kijeshi wa Marekani, Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani, alitangaza azma thabiti na aliyosema "isiyoweza kutenguliwa" iliyonayo serikali yake, ya kuwafukuza wavamizi wa Marekani; na makundi ya Muqawama ya nchi hiyo yakaitaka serikali itoe hakikisho la kutimiza ahadi hiyo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, maafisa wa Pentagon wametangaza kuwa katika muda wa siku 10 zilizopita, vikosi vya Marekani vimeshambuliwa mara 17 nchini Iraq, Syria na katika Bahari Nyekundu.

Mashambulizi ya hivi majuzi katika kambi ya kijeshi ya Marekani yamefanywa wakati waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Anthony Blinken, alipokamilisha safari yake ya masaa machache mjini Baghdad na kukutana na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani aliyataka makundi ya Muqawama ya Iraq yasishambulie kambi na askari wa jeshi la Marekani katika eneo.

Kufuatia kushambuliwa kwa makombora na jeshi la utawala wa Kizayuni hospitali ya Al-Ma'amadani huko Gaza, Muqawama wa Kiislamu wa Iraq uliionya Marekani kwamba kuanzia hapo utavishambulia vituo vya jeshi la nchi hiyo vilivyoko katika ardhi ya Iraq.../

 

Tags