Jan 22, 2024 12:02 UTC
  • Hujuma za Israel zimebomoa misikiti 1,000 Gaza tokea Oktoba 7

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Dini katika Ukanda wa Gaza imesema mashambulizi ya vikosi vya utawala katili wa Israel dhidi ya eneo hilo lililozingirwa yamebomoa na kuharibu misikiti 1,000 tokea Oktoba 7 mwaka uliopita hadi sasa.

Ofisi ya Habari ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imeinukuu Wizara ya Wakfu na Masuala ya Dini katika ukanda huo ikisema kuwa, tangu Oktoba 7, 2023, jeshi la Israel limeharibu misikiti 1,000 kati ya 1,200 inayopatikana katika eneo hilo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.

Wizara  hiyo imesema kuikaribati misikiti hiyo kutahitaji zaidi ya dola milioni 500. Imeelezwa kuwa, baadhi ya maeneo hayo ya ibada ni turathi za kihistoria na yana ukongwe wa zaidi ya miaka 1000.

Aidha vikosi vya utawala haramu wa Israel vimeharibu na kuvunjia heshima makumi ya makaburi katika Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7 hadi sasa, mbali na kushambulia pia makanisa.

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Dini ya Gaza imeripoti kuwa, Kanisa la Kiothodoksi ambalo ni kongwe na la kihistoria ni miongoni mwa makanisa yaliyoharibiwa na hujuma hizo za Israel huko Gaza.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yamepelekea kuuawa shahidi wanazuoni, wahubiri, maimamu, na waadhini zaidi ya 100 tangu Oktoba 7 hadi sasa.

Kadhalika hujuma hizo za Israel dhidi ya Gaza zimeripotiwa kulenga ofisi za kamati za kukusanya zaka, madrasa za Qurani na makao makuu ya Benki ya Wakfu.

Hii ni katika hali ambayo, shirika huru la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Rights Monitor limeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewauwa shahidi maprofesa 94 wa vyuo vikuu, mamia ya walimu, na maelfu ya wanafunzi katika Ukanda wa Gaza katika muda wa miezi mitatu iliyopita.

Tags