Jul 12, 2016 17:02 UTC
  • Utawala wa Saudia wamkamata mwanazuoni mkubwa wa Kishia

Saudi Arabia imemkamata mwanazuoni mkubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo, huku utawala huo wa kifalme ukiendelea kubana harakati za kidini za raia wa maeneo ya mashariki yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Ripoti zinasema kuwa, utawala wa Saudia umemkamata Sheikh Mohammad Hassan al-Habib, katika eneo la Safavi kwenye mkoa wa Qatif.

Wakazi wa eneo hilo wanasema, Sheikh al Habib pamoja na wenzake watatu walikamatwa Jumamosi iliyopita na kupelekwa kwenye vyombo vya usalama mjini Riyadh kwa ajili ya kusailiwa.

Familia ya Sheikh Mohammad Hassan al-Habib inasema haijapewa taarifa yoyote kuhusu hatima ya msomi huyo wala mahala anakoshikiliwa.

Sheikh Mohammad Hassan al-Habib anajulikana katika eneo lenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia la Qatif kwa ukosoaji wake mkubwa dhidi ya serikali ya kifalme ya Saudi Arabia na sera zake za kuwakandamiza Waislamu wa Kishia. Mwanazuoni huo alizidisha ukosoaji wake mkubwa katika hotuba alizotoa baada ya serikali ya Saudia kumnyonga Ayatullah Nimr Baqir al-Nimr na wanaharakati kadhaa wa eneo la mashariki mwa Saudia mapema mwaka huu.

Mauaji ya Ayatullah Nimr na wanaharakati wenzake yalizusha malalamiko makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati ya duniani kote na kuakisi tena dhulma na manyanyaso wanayokumbana nayo Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudia.

Tags