May 10, 2024 07:24 UTC
  • Muqawama wa Iraq washambulia maeneo ya kistratajia ya Israel, Eilat

Harakati ya Kiislamu ya Iraq imetangaza kuwa imeshambulia maeneo ya kistratajia ya Israel katika mji wa Eilat, ulioko kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tovuti ya habari ya Press TV imeripot habari hiyo na kuongeza kuwa, wanamuqawama hao wa Iraq leo Ijumaa wamefanya operesheni dhidi ya eneo la kistratajia la Israeli katika bandari ya Eilat, kaskazini mwa ncha ya Bahari Nyekundu.

Harakati hiyo ya muqawama ya Iraq imesema imefanya operesheni hiyo katika muendelezo wa kupinga mashambulizi ya utawala haramu wa Israel, kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza, na kukabiliana na mauaji yanayofanywa dhidi ya raia wa Palestina, wakiwemo watoto, wanawake na wazee.

Kabla ya hapo, muqawama wa Iraq ulisema kuwa umefanya operesheni nyingine dhidi ya kambi ya anga ya Ovda kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israeli.

Wapiganaji wa Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq wamesisitiza kuwa wataendeleza operesheni zake dhidi ya maeneo ya utawala haramu wa Israel, madhali utawala huo katili unaendelea kumwaga damu za Wapalestina.

Wapiganaji wa Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq

Muungano wa makundi ya muqawama nchini Iraq umekuwa ukifanya mashambulizi mengi kama hayo dhidi ya maeneo ya utawala wa Israel, tangu utawala huo unaoikalia kwa mabavu Palestina, uanzishe vita na mauaji ya halaiki huko ukanda wa Gaza mwezi Oktoba 7 mwaka jana 2023.

Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, utawala huo haramu wa Israel umeua Wapalestina karibu 35,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

 

Tags