May 24, 2024 07:22 UTC
  • Hizbullah, Harakati ya Muqawama Iraq zashambulia ngome za Israel

Wanamapambano wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq wamefanya operesheni tofauti dhidi ya kambi na ngome za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel, katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu mwaka 1948, kwa ajili ya kulipiza kisasi cha vita vya umwagaji damu vya Israel dhidi ya Gaza.

Televisheni ya al-Mayadeen imeripoti kuwa, wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon wameshambulia mikusanyiko ya wanajeshi wa Israel kwenye vituo vya kijeshi katika kijiji cha Even Menachem, magharibi mwa al-Jalil (Galilee). 

Aidha wanajihadi wa Hizbullah wameshambulia pia mkusanyiko wa wanajeshi wa Israel katika kambi ya kijeshi ya Israel mkabala wa kijiji cha kusini mwa Lebanon cha Yaroun, kwa kutumia makombora.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeapa kuendeleza operesheni zake za kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendeleza mauaji ya kimbari huko Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo, wanajihadi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq wameshambulia maeneo ya kistratajia ya Israel katika maeneo ya kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Wanajihadi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq

Habari zaidi zinasema kuwa, wanamuqawama hao wameshambulia ngome za Israel katika mji wa bandari wa Haifa, kwa kutumia droni ya kamikaze. Aidha wapiganaji wa kundi hilo la muqawama wa Iraq walilenga kwa makombora vifaru na magari ya kijeshi ya Israel, ambayo yalikuwa na vifaa vya ujasusi.

Harakati hiyo ya muqawama ya Iraq imesema imefanya operesheni hiyo katika muendelezo wa kupinga mashambulizi ya utawala haramu wa Israel, kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza, na kukabiliana na mauaji yanayofanywa dhidi ya raia wa Palestina, wakiwemo watoto, wanawake na wazee.

Tags