Ansarullah: Jinai za Israel ni mtihani hatari kwa jamii ya mwanadamu
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu mwezi Oktoba 2023 ni mtihani hatari mno kwa jamii ya mwanadamu.
Sayyid Abdul Malik al Houthi ameelezea kusikitishwa mno na kimya cha jamii ya kimataifa duniani mbele ya jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, kimya hicho ni ushahidi wa kutoweka kabisa heshima ya mwanadamu na haki ya kuishi jamii za binadamu hapa duniani.
Kiongozi huyo huyo wa Ansarullah ya Yemen ameongeza kuwa, jinai zinazofanywa na Israel ni uvunjaji wa sheria zote za kimataifa na vitendo hivyo vinazidhalilisha jamii za mwanadamu.
Sayyid Abdul Malik al Houthi pia amesema kuwa maandamano makubwa ya wanafunzi wa vyuo vikuu duniani hasa wa nchini Marekani yamethibitisha kwamba watu huru duniani na wenye hisia za kibinadamu hawawezi kuvumilia hata chembe jinai hizo za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia.
Amesema, Marekani imekandamiza kikatili maandamano ya kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina wakati ilitakiwa iingie akili na iwe na hisia za kibinadamu na kuacha kusaidia jinai za Wazayuni huko Ghaza.