Kiongozi wa Hizbullah: Israel ni uvimbe wa saratani, utaondolewa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i114152-kiongozi_wa_hizbullah_israel_ni_uvimbe_wa_saratani_utaondolewa
Kiongozi wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema "uvimbe wa saratani" wa Israel utaondolewa na kizazi cha sasa cha Wapalestina.
(last modified 2024-07-17T03:16:04+00:00 )
Jul 17, 2024 03:16 UTC
  • Kiongozi wa Hizbullah: Israel ni uvimbe wa saratani, utaondolewa

Kiongozi wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema "uvimbe wa saratani" wa Israel utaondolewa na kizazi cha sasa cha Wapalestina.

Akuzungumza jana Jumanne kupitia televisheni ya harakati hiyo, Sayyid Hassan Nasrullah amesema, "Mwenyezi Mungu atateremsha adhabu yake kwa utawala huu ghasibu kupitia watu wanaoamini kuwa Israel ni uvimbe wa saratani ambao lazima uondolewe." Nasrullah aliyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa Siku ya Ashura nchini Lebanon. Ashura ni ukumbusho wa kuuawa shahidi Imam Hussein (as), Imam wa tatu wa Shia na ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Nasrullah ameongeza kuwa wataalamu wa masuala ya kisiasa wanasema Israel inaweza kuishi kwa miaka 80 pekee na kwamba hali yake ya sasa inaashiria kusambaratika utawala huo.

Amesema: "Wasomi wa utawala wa adui wanakadiria kuwa utawala huo utatoweka kati ya miaka 70 hadi 80 baada ya kuanzishwa, na takwimu zao za asili, kihistoria na kijamii zinaonyesha kuwa utawala huo umefikia hatua nyeti."

Hassan Nasrullah ameendelea kusema: "Vizazi vya sasa vya Gaza na waungaji mkono wao, Mungu akipenda, ndivyo vitaiangamiza Israel, na kama Waarabu wangeruhusiwa na mipaka kufunguliwa, tungewaona wakitimiza wajibu wao wa kuisaidia Gaza." Amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ya Oktoba 7 imekuwa na taathira nyingi chanya katika kupunguza mivutano ya kimadhehebu iliyotwishwa eneo la Asia Magharibi.

Nasrallah ameyatuhumu mashirika ya kijasusi ya Magharibi kwa kuchochea mizozo ya kimadhehebu katika eneo tangu miaka kumi iliyopita. Amesema, baadhi ya nchi ambazo zimekataa kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza zimekuwa zikichochea tofauti za kimadhehebu katika eneo.

Mashambulio ya Hizbullah katika maeneo ya walowezi wa Kizayuni

Ameyataja yaliyotokea katika eneo la Asia Magharibi tangu mwaka 1948 kuwa ni ufisadi wa kutisha na kuongeza kuwa, adui Mzayuni amewadhalilisha Waarabu wote kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi.

Akiashiria Aya za Qur'ani Tukufu, kiongozi wa Hizbullah amesema:

"Tunasonga mbele kwenye njia ya kupata ushindi, na hatuogopi kifo wala kutishwa nacho. Kwa wale wanaojaribu kututisha kuwa tutauawa na Marekani, Israel, Magharibi na wengine kutoka ndani, sisi ni watu ambao hatuogopi vita wala kutishwa navyo kwa sababu baya zaidi linaloweza kusababishwa na vita ni kifo, ambacho kwetu sisi ni ushindi wa kufa shahidi."

Hizbullah na Israel zimekuwa zikipigana tangu Oktoba mwaka jana, muda mfupi baada ya utawala huo ghasibu kuanzisha vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza kufuatia operesheni ya kushtukiza ya kundi la muqawama la Hamas huko Palestina.

Hizbullah imeapa kuendeleza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi maadamu utawala wa Tel Aviv unaendeleza vita hivyo ambavyo kufikia sasa vimeua Wapalestina wasiopungua 38,443 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na kupelekea wengine 88,481 kujeruhiwa.

Vyombo vya habari vya Israel vinasema kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Hizbullah yamewakosesha makaazi walowezi wapatao 60,000 katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.