Lavrov: Hizbullah, serikali ya Lebanon hawataki vita kamili na Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov, amesema harakati ya Hizbullah ya Lebanon na serikali ya nchi hiyo hawataki "vita kamili" na Israel lakini baadhi ndani ya utawala huo wa Israel wanataka vita.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia amesema "kuna ishara kwamba baadhi ya duru huko Israel zinajaribu kuanzisha vita kamili dhidi ya Lebanon."
Lavrov, amewanukuu baadhi ya wachambuzi wa Marekani na Ulaya, akisisitiza kwamba "kuna ishara kwamba Israel inavutiwa na vita dhidi ya Lebanon."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuna vitendo vya makusudi vya kuiburuta Hizbullah katika vita licha ya kiongozi wa harakati hiyo kusema wazi kwamba hawataki kuingia katika vita kamili. Hata hivyo Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa harakati hiyo iko tayari kujilinda iwapo Israel itaanzisha vita kamili dhidi ya Lebanon.
Hizbullah pia imeapa kuendeleza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel maadamu utawala huo katili unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo Sergei Lavrov amesisitiza kwamba mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza yamevuka mipaka na sasa ni aina ya "adhabu ya pamoja" kwa Wapalestina milioni 2.3 wa eneo hilo.
Utawala wa Tel Aviv umewauwa shahidi takriban Wapalestina 38,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, huko Gaza, tangu Oktoba 7 mwaka jana.