Kufeli njama za kuleta fitna baina ya Waislamu nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i114258-kufeli_njama_za_kuleta_fitna_baina_ya_waislamu_nchini_afghanistan
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan ametangaza kuwa, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, kumefanyika njama nyingi za kuzusha fitna baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia nchini humo lakini zote zimefeli.
(last modified 2024-07-19T22:48:46+00:00 )
Jul 19, 2024 22:48 UTC
  • Kufeli njama za kuleta fitna baina ya Waislamu nchini Afghanistan

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan ametangaza kuwa, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, kumefanyika njama nyingi za kuzusha fitna baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia nchini humo lakini zote zimefeli.

Amir Khan Muttaqi amegusia namna maombolezo ya Muharram yalivyofanyika kwa mafanikio na kwa utulivu mkubwa mwaka huu nchini Afghanistan bila ya kuweko tukio lolote la kigaidi na kusisitiza kuwa, hivi sasa mizozo baina ya madhehebu za Kiislamu nchini Afghanistan imeisha. Amesema: Katika kipindi cha miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu Aghanistan na madola ya kibeberu ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, maadui hao walifanya njama chungu nzima za kuzusha na kuimarisha mifarakano baina ya Mashia na Masuni, lakini njama hizo zimeshindwa na hivi sasa watu wa makabila na madhehebu zote wanaishi kwa salama baina yao nchini Afghanistan. 

Hali ya Ashura nchini Afghanistan mwaka 2024

Matamshi ya Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan yamekuja ikiwa ni kuashiria kipindi cha miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO likiongozwa na Marekani. Suala la kwamba Waislamu wa Kisuni na Kishia wamekuwa wakiishi kwa salama na amani nchini Afghanistan na kwenye eneo hili zima katika kipindi chote cha historia, ni jambo ambalo halina shaka yoyote. Hii ni kwa sababu, Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW akiwemo Imam Husain AS, wanapendwa na Waislamu wa madhehebu yote, tab'an kuna kuzidiana katika mapenzi ya Ahlul Bayt, lakini kila Muislamu anawapenda watu wa nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Ushahidi wa hayo ni kwamba, majina kama Ali, Hassan, Husain, Fatma na Zainab ni miongoni mwa majina yanayopendwa na Waislamu wa jamii zote duniani bila ya kujali madhehebu zao.

Amin Farhad, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Moja ya mambo yanayoleta umoja na mshikamano kati ya wananchi wa Afghanistan ni kuheshimu dini na madhehebu za wengine, na sifa hiyo ina historia kongwe kati ya wananchi wa Afghanistan. Kwa kweli moja ya sifa nzuri za wananchi wa Afghanistan ni suala hili la kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana watu wa imani na itikadi tofauti. Ndio maana muda wote wa vita vya ndani, vita hivyo kamwe havikuwa na sura ya kidini na kimadhehebu; vilikuwa tu na sura ya kikabila na kikaumu."

Hali ya Muharram mjini Ghazni Afghanistan

 

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan amesema kuhusu sheria zilizowekwa wakati wa mwezi wa Muharraam mwaka huu na kusisitiza kuwa, katika kipindi cha miaka 20 iliypita, baadhi ya watu walitumia maombolezo ya mwezi wa Muharram kwa malengo yao ya kisiasa na kiuchumi na ndio maana misafara na maandamano ya maombolezo ya Muharram ilikuwa miaka yote inafuatiwa na magari ya wagonjwa kwa ajili ya kukusanya miili na majeruhi walioshambuliwa kwa miripuko ya mabomu na magaidi wasiolitakia kheri taifa la Afghanistan. Lakini mwaka huu hakuna tukio hata moja la kigaidi lililotokea wakati wa maombolezo hayo ya Muharram. Amesema huu ni ushahidi kwamba waliokuwa wanafanya mashambulizi hayo walikuwa ni wageni kutoka nje si wananchi halisi wa Afghanistan na lengo lao lilikuwa ni kuzusha fitna baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia na kuhakikisha usalama na amani inapotoea nchini Afghanistan. Mara zote genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh yaani ISIS ndilo lililokuwa linatangaza kuhusika na jinai hizo za kigaidi. Kaimu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Aghanistan pia amesema kuwa, iwapo vituo vya magaidi wa Daesh katika nchi za nje vitandelea kuwepo, basi lazima tutarajie kuendelea kutokea mashambulizi ya kigaidi sehemu mbalimbali ikiwemo Afghanistan. Mtazamo wa  Amir Khan Muttaqi, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan ni kwamba ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni muhimu sana katika kuwaangamiza magaidi wa ISIS.

Alaakullihaal, onyo hilo la Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan inabidi lichukuliwe kwa uzito na nchi zote za eneo hili kwani hofu kubwa iliyopo hivi sasa ni kwamba baada ya kutimuliwa Marekani huko Afghanistan, dola hilo la kibeberu na mengineyo lazima yatafanya njama za kuhakikisha kuwa Afghanistan inaendelea kuwa maficho salama ya magaidi ambao wanahatarisha usalama wa eneo hili na dunia nzima kwa ujumla.