Hizbullah ya Lebanon yashambulia vitongoji vya Wazayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena imekishambulia kwa makombora kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Dona, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).
Harakati ya Hizbullah jana ilitoa taarifa na kutangaza kuwa, imejibu jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia kusini mwa Lebanon khususan jinai zilizofanywa na utawala huo katika kitongoji cha Adlun kwa kukishambulia kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Dona kwa makombora ya katyusha huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na katika kuwaunga mkono Wapalestina.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon hivi karibuni alitoa onyo kwa Wazayuni wakati alipohutubia marasimu ya Ashura huko Beirut kwamba: Muqawama wa nchi yake utavishambulia vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni ambavyo hadi sasa havijalengwa na mashambulizi.

Tangu kuanza operesheni za Hizbullah huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel); walowezi wengi wa Kizayuni katika eneo hilo wamelazimika kuyahama makazi yao, na kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Kizayuni, aghlabu ya wakazi waliosalia katika eneo hilo wanasumbuliwa na matatizo ya kiakili na kisaikolojia.