Ansarullah yasema itachukua hatua kali za kulipiza kisasi dhidi ya Israel
Afisa wa ngazi ya juu wa Yemen amesema nchi hiyo italipiza kisasi kwa shambulio baya la hivi karibuni la anga dhidi ya al-Hudaydah, na kwamba Israel lazima iwe tayari kwa matukio yasiyotarajiwa katika siku zijazo.
Ali al-Qahoum, afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, katika taarifa yake siku ya Jumanne amesema kuwa jibu la mashambulizi ya Israel yaliyolenga bandari ya Hudaydah Jumamosi iliyopita halitacheleweshwa.
Al-Qahoum ameuonya utawala wa Israel kwamba jibu la Yemen "lisiloweza kuepukika, lenye nguvu na la kukandamiza" litakuwa tetemeko la ardhi kwa utawala huo ghasibu.
Pia amewashauri Waisraeli wasifurahi sana, kwani hakuna njia ya kuepuka adhabu. Aidha ameufahamisha utawala wa Israel kwamba uungaji mkono wa Marekani na Uingereza hautakuwa na faida.
Siku ya Jumamosi ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zililenga majengo, vituo vya mafuta na kituo cha kuzalisha umeme huko Hudaydah na kuua takriban watu sita.
Uchokozi huo ulikuja siku moja baada ya Wanajeshi wa Yemen kufanya shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye eneo karibu na ubalozi wa Marekani huko Tel Aviv katika kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Maafisa wa Yemen wametangaza mara kwa mara kwamba hawatasitisha mashambulizi yao maadamu Israel inaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza, ambayo yameua takriban watu 39,006 na kuwajeruhi wengine 89,818.