Baghdad: Wanajeshi wote wa Marekani waondoke Iraq kufikia mwakani mwishoni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i114448-baghdad_wanajeshi_wote_wa_marekani_waondoke_iraq_kufikia_mwakani_mwishoni
Ujumbe wa Iraq katika mazungumzo ya pamoja ya usalama na Marekani umetoa pendekezo la kuondoka nchini Iraq wanajeshi wote wa Marekani ifikapo mwiishoni mwa mwaka ujao.
(last modified 2024-07-25T03:33:19+00:00 )
Jul 25, 2024 03:33 UTC
  • Baghdad: Wanajeshi wote wa Marekani waondoke Iraq kufikia mwakani mwishoni

Ujumbe wa Iraq katika mazungumzo ya pamoja ya usalama na Marekani umetoa pendekezo la kuondoka nchini Iraq wanajeshi wote wa Marekani ifikapo mwiishoni mwa mwaka ujao.

Pendekezo hilo limetolewa wakati wa mazungumzo ya pande mbili ya usalama kati ya Iraq na Marekani katika jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon. Kwa mujibu wa pendekezo hilo, zoezi la kuondoka wanajeshi wa Marekani walioko nchini linapaswa kuanza Septemba mwaka huu na kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao wa 2025.

Tangu mwaka 2014, takriban wanajeshi 2,500 wa Marekani wamekuwepo nchini Iraq kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daes, na wanajeshi hao wamesambazwa katika vituo vitatu kuu: Ain al-Asad mjini Anbar, Harir mjini Erbil, na Camp Victory jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. 

Jumbe za Marekani na Iraq zikiwa katika mazungumzo ya pamoja ya usalama

 

Mazungumzo kati ya Baghdad na Washington yalianza Februari mwaka huu kwa kupasishwa upunguzaji wa hatua kwa hatua wa idadi ya vikosi vya eti muungano wa kimataifa dhidi ya Daesh na hatimaye kumaliza kazi ya vikosi hivyo, na duru mbili zingine za mazungumzo hayo zilifanyika katika miezi ya Machi na Aprili.

Wakati Baghdad inasisitiza juu ya ulazima wa kuhitimishwa operesheni za muungano wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, ni jambo lililo mbali katika mazingira ya sasa ambapo Marekani inajiandaa na uchaguzi wa Rais kuiona ikikubali kutia saini makubaliano ya kuondoka kwa vikosi vyake kutoka Iraq.