Mateka wa Kipalestina; kuendelea muqawama sambamba na kushadidi ukatili wa Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i114576-mateka_wa_kipalestina_kuendelea_muqawama_sambamba_na_kushadidi_ukatili_wa_wazayuni
Katika hali ambayo, utumiaji mabavu na ukatili wa Wazayuni dhidi ya mateka wa Kipalestina umechukua mkondo na wigo mpana zaidi, mateka wa Kipalestina wameshikamana na muqawama na njia ya kufa shahidi.
(last modified 2024-07-28T11:02:17+00:00 )
Jul 28, 2024 11:02 UTC
  • Mateka wa Kipalestina; kuendelea muqawama sambamba na kushadidi ukatili wa Wazayuni

Katika hali ambayo, utumiaji mabavu na ukatili wa Wazayuni dhidi ya mateka wa Kipalestina umechukua mkondo na wigo mpana zaidi, mateka wa Kipalestina wameshikamana na muqawama na njia ya kufa shahidi.

Utawala unaokalia kwa mabavu Baytul-Muqaddas kuanzia mwaka 1948 hadi sasa umewatia mbaroni maelfu ya Wapalestina. Tangu kuanzishwa kwake, utawala huo umekuwa ukitumia kila aina ya mbinu zisizo za kibinadamu katika kukabiliana na Wapalestina.

Baadhi ya mateka hao wamekaa miaka mingi katika magereza ya kuogofya Wazayuni bila kufunguliiwa kesi. Wengine wameachiliwa, wengine bado wamezuiliwa na wengine wameuawa shahidi.

Klabu ya Mateka wa Palestina imetangaza kuwa, mateka 256 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika jela za utawala wa Kizayuni tangu mwaka 1967. Asasi hiyo imefafanua kuwa, idadi hiyo inajumuisha mashahidi ambao utambulisho wao umejulikana. Fauka ya hayo kuna, makumi ya mateka wa Kipalestina waliouawa shahidi kwa kunyongwa kwa umati hadharani huko Gaza na jeshi la utawala wa Kizayuni, na hakuna takwimu za kuaminika kuhusiana na utambulisho wao wala idadi yao.

 

Baada ya operesheni ya kishujaa ya kimbunga cha Al-Aqswa mnamo Oktoba 7, 2023, utumiaji mabavu na ukatili dhidi ya mateka wa Kipalestina umeongezeka mno. Lishe isiyofaa na inayo ya kibinadamu, mateso ya usiku, kuachiliwa mbwa kuwabughudhi mateka wa Kipalestina, kupigwa, mateso ya kuchomwa na shoti ya umeme, familia za mateka kutokuwa na taarifa za wapendwa wao na kuwadhalilisha ni miongoni mwa mbinu na njia zisizofaa na zisizo za kiutu, zinazotumiwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya mateka wa Kipalestina.

Abu Salimah, Mkurugenzii wa Hospitali ya al-Shifaa ambaye hivi karibuni aliachiwa kutoka katika gereza la Wazayuni anasema:

“Mateka wako katika hali mbaya ambayo taifa la Palestina halijawahi kuishuhudia tangu mwaka 1947; mateka wapya na wa zamani wote wanakabiliwa na udhalilishaji wa  kimwili na wanataabika mno kupata chakula na maji, muqawama lazima uwe na sauti ya mwisho katika kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina."

Katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, idadi ya mateka  wa Kipalestina waliouawa shahidi kutokana na kuteswa, ambapo tukio la hivi karibuni kabisa ni kuuawa shahidi, Sheikh Mustafa Abu Ara, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika jela ya Utawala vamizi wa Kizayuni imeongezeka mno.

 

Mateka wa Kipalestina wameendelea kusimama kidete licha ya ukatili wa Wazayuni

Kuuawa shahidi kiongozi huyo wa Hamas, kunaifanya idadi ya mateka wa Kipalestina waliokufa shahidi chini ya mateso katika jela za utawala wa Kizayuni tangu kuanza kwa vita dhidi ya Gaza Oktoba 7 mwaka jana kuongezeka na kufikia watu 19.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, baada ya operesheni ya kimbunga cha Al-Aqswa, idadi ya mateka wa Kipalestina imeongezeka sana. Ongezeko hili ni kubwa kiasi kwamba, baraza la mawaziri la Kizayuni linajaribu kuanzisha takriban vituo 1000 vya kuwazuilia mateka wa Kipalestina.

Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala haramu wa Israel, hivi karibunii aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: Kunyonga ndio ufumbuzi wa kutatua tatizo la msongamano katika magereza. Waziri huyo mwenye misimamo ya kuufurutu ada katika serikali ya Israel akitoa radiamali yake kwa hatua ya baraza la mawaziri la Israel ya kuafiki kujengwa takribani vituo vingine 1000 kwa ajili ya kuwashikilia mateka wa Kipalestiina alionyesha kufurahishwa sana na uamuzi huo.

 

Nukta ya mwisho ni kuwa, licha ya kushtadi kwa ukatili wa Wazayuni dhidi ya mateka wa Kipalestina, lakini mateka hao wameshikamana na njia ya muqawama na hawaogopi kuuawa shahidi. Msimamo huo umewakasirisha sana Wazayuni kwa sababu walitarajia kwamba mateka hao watasalimu amri hasa baada ya kushadidishwa vitendo vya utumiaji mabavu na ukatili dhidi yao. Lakini kinyume na matarajio yao, mateka hao wamesimama kidete na kuonyesha azma yao thabiti ya kuunga mkono muqawama na mapambano dhidi ya Israel hata kama hilo litawagharimu maisha yao.