Nusu ya watoto wa Yemen wanasumbuliwa na utapiamlo wa muda mrefu
Waziri Mkuu wa Yemen, Ahmed Awad bin Mubarak, amefichua kuwa asilimia 50 ya watoto wa nchi hiyo wanasumbuliwa na utapiamlo wa muda mrefu, na kwamba asilimia 21 kati yao wanakabiliwa na udumavu kutokana na tatizo hilo.
Ahmed Awad bin Mubarak amesema katika mji wa Aden kwamba changamoto zinazoikabili serikali katika suala la idadi ya watu ni kwamba 45% ya watu wana umri wa chini ya miaka 16, wakati 50% ya watoto wanasumbuliwa na utapiamlo sugu, na 21% kati yao wanakabiliwa na udumavu.
Bin Mubarak amedokeza kwamba hatari ya takwimu hizi inazidisha ulazima wa kushughulikiwa kwa umakini na kuzipa kipaumbele katika mipango, programu na matumizi yote.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema idadi ya watu nchini Yemen ni takriban milioni 32, wengi wao wakihitaji msaada wa kibinadamu.
Kwa miaka miwili sasa, Yemen inashuhudia hali ya utulivu wa kiwango fulani baada ya vita vya takriban miaka 10 vya Saudi Arabia na washirika wake wa Kiarabu na Kimagharibi dhidi ya taifa hilo la Kiislamu.