OXFAM yaonya kuhusu kuendelea jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza
Shirika la Misaada ya Kibinadamu la OXFAM limeonya kuhusiana na kuendelea jinai za utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza limetabiri katika ripoti iliyochapishwa jana kwamba, ikiwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yataendelea bila kusimama wakati wa likizo ya majira ya joto ya Bunge la Uingereza, takriban watu elfu saba watauawa shahidi katika ukanda huo au watajeruhiwa .
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, katika likizo hiyo ya siku 33 ya Bunge la Uingereza, huenda watu 1800 wakiwemo zaidi ya watoto 600 wataongezwa kwenye idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, na zaidi ya watu elfu 5 watajeruhiwa.
Wakati huo huo mashirika ya kutetea haki za binadamu yameikosoa serikali ya Uingereza kwa kuendeleza siasa za kuuzia silaha utawala wa Kizayuni na kushiriki katika ukiukaji wa sheria za kimataifa na za kibinadamu unaofanywa na utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripoti mpya ya pamoja iliyotolewa na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Ukanda Ghaza uliowekewa mzingiro na kuzuiliwa na jeshi la Kizayuni kuingiziwa misaada ya chakula, ndilo eneo linalokabiliwa na hali mbaya zaidi ya ukosefu wa chakula duniani.