Shahidi Haniyeh; mwanamapambano imara na shupavu
Shahidi Ismail Haniyeh Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) alikuwa mwanamapambano ambaye alijitolea maisha yake yote katika kuendesha mapambano dhidi ya maadui wa Uislamu.
Ismail Haniyeh alikuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambaye Mei 6 mwaka 2017 alishika wadhifa wa Mkuu Mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas akichukua nafasi ya mtangulizi wake Khalid Mash'aal.
Ismail Abdulsalam Ahmad Haniyeh maarufu kwa lakabu ya Abu Abdusalam alizaliwa tarehe 23 mwezi Mei 1962 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya al Shati. Familia yake ilihamishwa kwa nguvu katika kijiji cha "Jurah" huko Ashkelon, katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu ya Palestina mnamo mwaka 1948. Alitunukiwa shahada ya udaktari wa heshima katika Chuo Kikuu cha Kiislamu katika Jiji la Gaza mwaka 2009; alioa na kujaaliwa watoto 13.
Haniyeh alifuzu elimu yake ya msingi na sekondari katika shule za UNRWA na alitunukiwa diploma yake kutoka Kituo cha Al-Azhar; na kisha mwaka 1981 alianza masomo katika Chuo Kikuu cha Kiislamu katika mji wa Gaza ambapo alihitimu katika masomo ya fasihi ya lugha ya Kiarabu.
Ismail Haniyeh alikuwa na kazi na majukumu mengine mengi katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza kabla ya kuwa mjumbe wa kamati ya uongozi wa chuo hicho mwaka 1997. Alikuwa Mkuu wa Ofisi ya Sheikh Ahmad Yassin baada ya kuachiwa huru Sheikh Yassin.
Haniyeh pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ngazi ya Juu ya Majadiliano na Mwakilishi wa Hamas katika kamati kuu ya kufuatilia masuala ya makundi ya kitaifa na Kiislamu wakati wa Intifadha ya Pili.
Utawala wa Kizayuni kwa mara ya kwanza mwaka 1987 na baada ya kupamba moto vuguvugu la Intifadha ya Kwanza ya Palestina ulimtia nguvuni Haniyeh na kumshikilia kwa siku18.
Mwaka 1988 Ismail Haniyeh alikamatwa na kufungwa jela kwa mara ya pili kwa muda wa miezi sita. Mwaka 1989 pia Haniyeh alitiwa nguvuni akituhumiwa kuwa mwanachama wa Hamas na kisha kufungwa jela ambako alisalia huko kwa miaka mitatu. Kisha Haniyeh pamoja na viongozi wemgine 415 wa Palestina khususan viongozi wa harakati za Hamas na Jihadul Islami walibaidishwa katika eneo la Marj al-Zhour huko Lebabon na baadaye alirejea Gaza baada ya mwaka mmoja.
Tarehe 6 Septemba 2003 Ismail Haniyeh alinusurika kuuawa katika oparesheni ya kigaidi ambapo utawala wa Kizayuni ulikusudia kumuuwa kiongozi huyo wa Hamas pamoja na Sheikh Ahmad Yassin.
Kisha aliingia bungeni kama Mkuu wa Orodha ya "Mabadiliko na Mageuzi" yenye mfungamano na harakati ya Hamas, ambayo ilishinda viti vingi katika uchaguzi wa bunge wa Januari 2006, na alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Palestina mwezi Februari 2006.
Hii ni katika hali ambayo tarehe 20 Oktoba 2006 Haniyeh na timu yake aliyokuwa amefuatana nayo walifyatuliwa risasi wakati wa machafuko huko Ukanda wa Gaza na mtu mmoja aliuliwa shahidi miongoni mwao.
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zilishambulia pia nyumba ya Haniyeh katika kambi ya al Shati katika vita vya siku 51 msimu wa kiangazi mwaka 2014. Hatimaye Ismail Haniyeh Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameuawa shahidi leo alfajiri Jumatano Julai 31, baada ya kushambuliwa makazi yake hapa mjini Tehran.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran itawafanya wavamizi wa magaidi kujutia kitendo chao hicho cha uoga.
Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo katika radiamali yake kuhusu mauaji ya mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Ismail Haniya.
Huku akilaani mauaji ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter): Mshikamano kati ya mataifa mawili yenye fahari ya Iran na Palestina utakuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali, na njia ya muqawama na kutetea wanaokandamizwa itakuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali.
Wakati huo huo, makundi ya muqawama wa Palestina yametoa taarifa ya kulaani mauaji dhidi ya Ismail Haniya.
Makundi ya mapambano na Muqawama, yamelaani kitendo cha kigaidi cha kuuawa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kufuatia shambulio dhidi ya sehemu alikofikia mjini Tehran.
Katika taarifa yake, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetuma salamu za rambirambi kwa taifa kubwa la Palestina, Umma wa Kiislamu na wa Kiarabu na watu wote huru duniani kutokana na kuuawa shahidi Ismail Haniyeh na kuongeza kuwa, Haniyeh ameuawa shahidi na Wazayuni akiwa mjini Tehran.
Taarifa ya Hamas imesema, Ismail Haniyeh aliuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya kihaini ya Wazayuni kwenye makazi yake mjini Tehran.
Moussa Abu Marzouq, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, amesema kwamba, mauaji hayo hayatapita hivi hivi bila jibu.
Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza katika taarifa yake kwamba, mauaji ya mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran ni jinai ya kigaidi na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.