Makumi ya wanachama wa Daesh waangamizwa na jeshi la Iraq
Makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wameuawa na jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati za wananchi wa nchi hiyo.
Jeshi la Iraq limetangaza kuwa, wanachama 50 wa genge hilo wameangamizwa kupitia operesheni za kulikomboa eneo la Albu Shajal, lililopo mjini Fallujah katika mkoa wa al-Anbar, magharibi mwa nchi hiyo. Jeshi la Iraq limeongeza kuwa, baadhi ya magaidi hao wana uraia wa Kiarabu na wengine wakiwa sio Waarabu. Wakati huo huo, Mahmud al-Jamili, kamanda wa jeshi la wananchi anayesimamia operesheni za kijeshi mjini Fallujah, ametangaza kuuawa matakfiri wengine tisa katikati ya mji huo, akiwemo kiongozi wa ngazi za juu wa kundi hilo la Daesh mwenye uraia wa Libya maarufu kwa jina la Abu Yusr ambaye ameuawa kwa kulipukiwa na bomu. Kwengineko, jeshi la Iraq limetuma askari zaidi katika mji wa Makhmur katika mkoa wa Nainawa, kama maandalizi ya kuanza kuukomboa mji wa Mosul, kutoka mikononi mwa kundi hilo la kigaidi. Akihutubia Mkutano wa Usalama Munich, Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi ameutaja mwaka huu wa 2016 kuwa mwaka wa mwisho wa uepo wa wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.