Utawala wa Kizayuni wamkamata Khatibu wa Msikiti wa al-Aqsa, kisa kutoa pole mauaji ya Shahidi Ismail Haniyeh
Utawala wa Kizayuni wa Israel umemkamata Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa kwa kutuma salamu za rambirambi kutokana na mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya Shahidi Ismail Haniyeh.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, baada ya Sheikh Ekrima Sa'id Sabri, Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa, kutuma salamu za rambirambi kutokana na kuuawa shahidi Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa, utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia nyumba yake huko al- Swaneh, Quds Tukufu na kumkamata.
Makumi ya maelfu ya Wapalestina wamemsalia Swala ya maiti ya ghaibu Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, katika Msikiti wa al-Aqsa ulioko katika Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na utawala katili wa Israel, licha ya vikwazo vya utawala wa Kizayuni.
Haniyeh aliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na utawala katili wa Israel kwenye makazi yake kaskazini mwa Tehran mapema Jumatano iliyopita.
Jana askari usalama wa utawala wa Kizayuni waliwazuia Wapalestina kuingia Msikiti wa Al-Aqsa kwa ajili ya kutekeleza Swala ya Ijumaa.
Licha ya vikwazo vya polisi wa Kizayuni, Waislamu elfu 30 waliswali Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa.