Ripoti: Israel imeiba zaidi ya miili 2,000 kutoka kwenye makaburi ya Gaza
Vikosi vya jeshi la Israel vimeiba zaidi ya miili 2,000 iliyofukuliwa kutoka kwenye makaburi mbalimbali katika ukanda wa Gaza, huku ripoti kutoka Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza zikisema baadhi ya maiti zimerudishwa baada ya majeshi ya Israel "kuvunjia heshima miili" ya marehemu hao.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza imesema kuwa Israel imeiba miili 2,000 ya Wapalestina tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7 na kurudisha baadhi ya maiti hizo kwa njia isiyo ya kibinadamu.
Katika muda wa siku 304 za mauaji ya halaiki, utawala vamizi wa Israel umeiba zaidi ya miili 2,000 ya mashahidi kutoka kwenye makumi ya makaburi katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza, ambayo utawala huo umeyaharibu na kuyafukua kwa matingatinga na magari ya kijeshi, tukio ambalo linakiuka ubinadamu na hisia za kibinadamu," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa "jeshi la utawala ghasibu wa Israel linadunisha na kuvunjia heshima utu wa miili ya mashahidi 89, na kuwakabidhi kama mifupa na maiti zilizoharibika."

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Huduma ya Dharura ya Kiraia ya Palestina huko Khan Yunis kusini mwa Gaza, Yamen Abu Suleiman, alisema jana Jumatatu kwamba "wamepokea miili 80 ndani ya mifuko 15, ambayo kila mmoja ulikuwa na zaidi ya mashahidi wanne."
Abu Suleiman ameongeza kuwa wanajeshi wa Israel hawakutoa taarifa zozote kuhusu miili hiyo, ikiwa ni pamoja na majina yao au mahali ilipopatikana au kuchukuliwa, jambo ambalo amesema ni "uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu."
Awali, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa kitendo kilichofanywa na utawala wa Kizayuni cha kukabidhi miili ya mashahidi zaidi ya 80 wa Kipalestina katika hali iliyoharibika kabisa kinaonyesha kiwango kisicho na kifani cha jinai za utawala huo.