Iran na Russia katika mkondo wa kuimarisha ushirikiano
(last modified Tue, 06 Aug 2024 14:12:34 GMT )
Aug 06, 2024 14:12 UTC
  • Iran na Russia katika mkondo wa kuimarisha ushirikiano

Jumatatu ya jana tarehe 5 Agosti, Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa la Shirikisho la Russia  aliwasili mjini Tehran kwa lengo la kuimarisha maingiliano na kuchunguza masuala ya kieneo, kimataifa na uhusiano wa pande mbili.

Katika muendelezo wa ushirikiano wa kistratijia kati ya Tehran na Moscow, ujumbe wa ngazi ya juu wa Russia ukiongozwa na "Sergei Shoigu", Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa la Russia uliwasili Tehran Jumatatu kwa mwaliko wa mwenzake wa Iran Ali Akbar Ahmadian.

 Akiwa hapa mjini Tehran, Shoigu amekutana na rais, mkuu wa majeshi na mwenyeji wake Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran. Katika mazungumzo hayo, kulijadiliwa masuala mbalimbali kama ushirikiano mpana wa pande mbili na uimarishaji wake kuanzia usalama hadi mipango ya kibiashara na kiuchumi, pamoja na masuala mbalimbali ya usalama wa kimataifa na kikanda.

Jana Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Baraza la Usalama la Russia Sergei Shoigu na kuitaja Russia kuwa ni "mshirika wa kimkakati" wa Jamhuri ya Kiislamu na akasisitiza kwamba, kupanuliwa uhusiano na Moscow ni kipaumbele cha juu cha sera za nje za serikali yake.

Pezeshkian sambamba na kutilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa kieneo na kimataifa kati ya Iran na Russia,  alieleza kwamba, Tehran inaamini kuwa, kipindi cha uongozi wa kakmbi moja wa baadhi ya madola, ikiwemo Marekani kimepitwa na wakati na ushirikiano kati ya Iran na Russia ni katika muelekeo wa kueneza ulimwengu wa ushirikiano wa pande kadhaa ambao utaimarisha zaidi usalama na amani duniani.

Mazungumzo ya Rais Pezeshkian na Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia

 

Sambamba na kukosoa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za magharibi zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu kwa jinai za utawala wa Kizayuni, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Tehran haitaki kupanua wigo wa vita na migogoro katika eneo na inaamini kuwa Israel itapata jibu la jinai na kiburi chake. Kwa upande wake, Sergei Shoigu, Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa la  Russia naye sanjari na kuitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa mmoja wa waitifaki wa kistratijia wa Russia katika eneo, na kueleza kuridhishwa kwake na juhudi za pamoja za pande mbili hizo amesema bayana kwamba, uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta zote unakua na kuna matarajio mazuri ya malengo ya kupanuliwa zaidi uhusiano uliopo.

Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia daima umekuwa ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni, na ziara za maafisa wakuu wa nchi hizo mbili huko Moscow na Tehran katika kipindi hiki zinaashiria uhusiano huu wa kistratijia wa kina na wa muda mrefu kwamba, haujaaathiriwa na njama za kuuvuruuga. Hapana shaka kuwa, serikali mpya inayoongozwa na Masoud Pezeshkian itaongeza mahusiano haya.

Tukitupia jicho mchakato wa upanuaji wa uhusiano kati ya nchi hizi mbili katika muongo uliopita tunaona  kuwa, hali ya kikanda na kimataifa inaufanya uhusiano huu uzidi kuwa wa kimkakati. Utendaji huu wa pamoja ni ishara ya mabadiliko muhimu katika kukabiliana na sera za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja katika uhusiano wa kimataifa. Mashinikizo ya Marekani na  nchi za Magharibi na upinzani dhidi ya misimamo ya pande kadhaa kwa masuala ya kieneo katika Asia ya Kati, Caucasus na Mashariki ya Kati ni miongoni mwa mambo yaliyopoelekea kuimarishwa uhusiano wa Iran na Russia katika miaka ya hivi karibuni.

Bendera za Iran na Russia

 

Kazem Jalali, balozi wa Iran nchini Russia anasema kuhusu umuhimu wa mpango jumuishi wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwamba: Kiwango cha sasa cha uhusiano na uga wa ushirikiano kati ya Iran na Russia ni zaidi ya miongo kadhaa iliyopita, hivyo hili linapaswa kushughulikiwa katika fremu ya mpango jumuishi wa ushirikiano.

Maslahi ya pamoja ya Iran na Russia katika kufungwa kambi za kijeshi za Marekani na nchi nyingine za Magharibi katika eneo la Asia Magharibi, kukabiliana na tishio la Daesh na ugaidi nchini Iraq na Syria, mvuto wa ushirikiano wa kijeshi na silaha, na vikwazo dhidi ya Russia kutokana na operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine na nchi hizo mbili kuwa katika hali sawa na kujaribu kuondosha vikwazo hivyo ni sababu nyingine na motisha ambazo zimezileta Iran na Russia karibu zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Makatibu wa Mabaraza ya Usalama wa Taifa ya Iran na Russia

 

Kuimarishwa ushirikiano kati ya Iran na Russia pia kuna umuhimu wa kistratijia hasa katika hali ambayo Marekani inajaribu kuzuia muungano na upanuzi wa uhusiano kati ya Iran na nchi za eneo hili. Ni kwa muktadha huo, ndio maana  viongozi wa kisiasa wa nchi hizo mbili wamefikia hitimisho kwamba ili kufikia malengo husika wanapaswa kuongeza mashirikiano na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili.

Kuimarishwa kwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Iran na Russia kunaweza kutathminiwa kama jibu la mahitaji ya pande zote katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kwa hakika siasa zenye changamoto za Marekani katika eneo zimeupa umuhimu zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili, na hii ni katika hali ambayo Iran na Russia zimeonyesha kuwa katika masuala ya usalama hazina nia ya kurejea nyuma mbele ya siasa za upande mmoja za  Marekani pamoja na hegemonia, utoaji amri na ubwanyenye wa Washington.

Tags