Nasrullah: Israel inaogopa majibu ya Iran, Hizbullah kwa jinai zake
(last modified Wed, 07 Aug 2024 06:52:25 GMT )
Aug 07, 2024 06:52 UTC
  • Nasrullah: Israel inaogopa majibu ya Iran, Hizbullah kwa jinai zake

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema misaada ya nchi za Magharibi kwa Israel ni ithibati kuwa utawala huo wa Kizayuni hauna uwezo wa kujilinda, na unatiwa kiwewe na majibu tarajiwa ya Iran na kambi ya muqawama kwa msururu wa mauaji ya kigaidi uliyoyafanya katika siku za karibu katika eneo.

Sayyid Hassan Nasrullah alisema hayo jana kwenye hotuba ya kumuenzi shahid Fuad Ali Shukr, mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon aliyeuawa kigaidi na Wazayuni wiki iliyopita.

Sayyid Nasrullah amebainisha kuwa, "Upelekaji wa silaha za Magharibi ili kuipa himaya Israel dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi unaonyesha kutokuwa na uwezo wa kujilinda Tel Aviv. Israel haina nguvu kama ilivyokuwa kabla ya vita hivi, na heshima na uwezo wake wa kijeshi hauko tena kama ulivyokuwa."

Amesema kuwalenga viongozi wa Hizbullah hakutadhoofisha azma na irada ya harakati hiyo ya kuendelea na njia yake, akisisitiza kwamba mauaji ya hivi karibuni hayatabadilisha dhati na asili ya msingi ya muqawama.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, mauaji ya hivi karibuni ya viongozi wa muqawama yamezidisha masaibu ya utawala ghasibu wa Israel, na hivyo kuchochea ongezeko la operesheni dhidi ya Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kukimbia Wazayuni kutoka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, wakihofia ulipizaji kisasi kutoka kwa Iran na Hizbullah.

Sayyid Nasrullah ameeleza bayana kuwa, utawala wa Kizayuni unapasa kusubiri majibu makali kutoka kwa kambi ya muqawama na kuongeza kuwa, hakuna shaka mrengo wa mapambano utapa ushindi.