Mbu vamizi azua hofu ya malaria kote barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140458-mbu_vamizi_azua_hofu_ya_malaria_kote_barani_afrika
Aina ya mbu vamizi inayoenea kwa kasi imezua hofu kote barani Afrika, huku wanasayansi wakionya kuwa inaweza kuchochea kuibuka upya kwa ugonjwa wa malaria katika miji mikubwa.
(last modified 2026-08-06T11:02:01+00:00 )
Aug 06, 2026 10:59 UTC
  • Mbu vamizi, Anopheles Stephensi
    Mbu vamizi, Anopheles Stephensi

Aina ya mbu vamizi inayoenea kwa kasi imezua hofu kote barani Afrika, huku wanasayansi wakionya kuwa inaweza kuchochea kuibuka upya kwa ugonjwa wa malaria katika miji mikubwa.

Mbu huyo anayejulikana kwa jina la 'Anopheles Stephensi', ni tofauti na spishi nyingine za mbu wa kawaida wanaoeneza ugonjwa wa malaria. Kuenea aina hii ya mbu katika maeneo ya mijini yenye msongamano mkubwa wa watu, na kuzaliana kwake kwenye vyombo vya maji karibu na nyumba na majengo hupelekea jitihada za kudhibiti aina hiyo ya mbu kuwa ngumu.

Jambo la kutia wasiwasi zaidi ni kwamba spishi hiyo ina uwezo wa kustahimili karibu kila aina ya dawa kuu ya kuua wadudu inayotumika sasa kupambana na mbu; jambo linalodhoofisha mojawapo ya mikakati madhubuti zaidi duniani ya kudhibiti ugonjwa wa malaria.

Wataalamu wa afya wana hofu kuwa kuenea kwa kasi kwa aina hii ya mbu kunaweza kuwaweka mamilioni ya watu katika hatari ya kuugua malaria hasa katika miji inayokua ya nchi za bara la Afrika ambako kihistoria malaria haikuwa ikijitokeza sana.

Kwa sasa, wanasayansi wanafanya bidii kutafuta njia mpya za kudhibiti mbu- kuanzia mbinu za kibiolojia hadi teknolojia bunifu na dawa za kuua wadudu za kizazi kipya.

Kadiri spishi hii ya mbu ya 'Anopheles Stephensi' inavyoenea; watafiti wametahadharisha kuwa hatua za haraka na ushirikiano wa nchi mbalimbali unahitajika ili kukabiliana na tishio hili kabla ya kushindwa kudhibitiwa.