Muqawama: Kuchaguliwa Sinwar kunaonyesha Israel imeshindwa kufikia malengo yake
(last modified Wed, 07 Aug 2024 10:51:30 GMT )
Aug 07, 2024 10:51 UTC
  • Muqawama: Kuchaguliwa Sinwar kunaonyesha Israel imeshindwa kufikia malengo yake

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema hatua ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kutangaza kumteua Yahya Sinwar kuwa mrithi wa Ismail Haniyah, aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS, kwa mara nyingine tena inathibitisha kuwa, malengo ya Wazayuni ya kuwaua kigaidi viongozi wa muqawama yamegonga mwamba.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano na Hizbullah imebainisha kuwa, Israel haitaweza kufikia malengo yake si katika Ukanda wa Gaza tu, lakini pia katika eneo la Asia Magharibi kwa ujumla, kupitia mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Wapalestina na viongozi wa muqawama.

Hizbullah imekaribisha kwa mikono mwili kuchaguliwa na Sinwar na kueleza kwamba: Uchaguzi wa Sinwar unatuma "ujumbe mzito" kwa Israel, Marekani na washirika wake kwamba HAMAS imeungana katika uamuzi wake, ipo imara katika kanuni zake na katika chaguzi zake muhimu, na imedhamiria kuendeleza njia yake ya muqawama.

Kadhalika Harakati ya Muqawama ya HAMAS imesema Wazayuni wanapaswa kutambua kwamba, ugaidi wao wa kinyama wa kuwaua kigaidi viongozi wa mrengo wa muqawama hauwezi kuwafanikishia malengo yao maovu.

Aidha Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina (PFLP) imesema jinai za Wazayuni dhidi ya muqawama na viongozi wake hazijakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuiimarisha kambi hiyo ya mapambano. Imeeleza kuwa: Siku baada ya siku tutaendelea kushuhudia jinsi kambi ya muqawama inavyozidi kuwa imara na hasira za mataifa ya dunia zinavyozidi kuongezeka dhidi ya utawala katili na pandikizi wa Israel.

Wakati huo huo, Harakati ya Ikwanul Muslimin imekaribisha kuchaguliwa Sinwar kuwa Kiongozi wa Kisiasa wa HAMAS na kusisitiza kuwa, uteuzi huo unaonyesha kuwa HAMAS imesisimama kidete katika kupigania ukombozi wa Palestina.

Nayo Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesema kuwa, uchaguzi huo wa Sinwar unaonyesha kuwa, HAMAS bado ina nguvu na mshikamano, na kwamba adui hajaweza kudhuru fremu na muundo wa harakati hiyo licha ya kufanya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Tags