Aug 09, 2024 10:10 UTC
  • UNICEF: Ghaza imegeuzwa makaburi ya watoto, hakuna mwisho wa mateso wanayopata

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umetangaza kuwa, Ukanda wa Ghaza umegeuzwa makaburi ya watoto wa Kipalestina na hakuna mwisho wa machungu na mateso wanayopata watoto hao.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, UNICEF imeeleza kuwa, vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza vimekuwa na taathira mbaya sana kwa watoto ikiwemo ya vifo; na kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, zaidi ya watoto 15,000 wameuawa na makumi ya maelfu wamejeruhiwa kutokana na mashambulio ya jeshi la utawala huo.
 
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umeongeza kuwa: idadi ya watoto waliotoweka au waliotenganishwa na familia zao kutokana na mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza huenda ikawa ni elfu 21.

UNICEF imefafanua kuwa, nusu ya Wapalestina milioni moja na laki tisa waliolazimika kuyahama makazi yao katika Ukanda wa Ghaza ni watoto. Mfuko huo wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa umesisitiza kwa kusema, "vita vya Israel dhidi ya Ghaza vingali vinaendelea na vita hivi havijawaacha salama hata watu dhaifu na walio hatarini zaidi kuathirika".

 
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala bandia wa Kizayuni umefanya mauaji makubwa katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina; na kimya jamii cha kimataifa na taasisi za kutetea haki za binadamu kuhusiana na jinai za utawala ghasibu wa Israel zimepelekea kuendelea mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa na mashine ya vita ya utawala haramu wa Kizayuni.
 
Wapalestina wapatao 40,000 wameshauawa shahidi hadi sasa tangu yalipoanza mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.../

Tags