Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine wataka kukomeshwa vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i115278-umoja_wa_mataifa_kwa_mara_nyingine_wataka_kukomeshwa_vita_gaza
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuongezeka watu wanaouawa huko Gaza kunatisha na hivyo ametoa mwito wa kukomeshwa mara moja ukatili huo.
(last modified 2024-08-16T00:53:39+00:00 )
Aug 16, 2024 00:53 UTC
  • Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine wataka kukomeshwa vita Gaza

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuongezeka watu wanaouawa huko Gaza kunatisha na hivyo ametoa mwito wa kukomeshwa mara moja ukatili huo.

Volker Türk alisema hayo jana Alkkhamisi na kuongeza kuwa, hivi sasa zaidi ya watu 40,000 wameshauawa katika Ukanda wa Gaza na jambo hili chungu linapaswa kuichochea dunia kuingilia kati kwa nguvu zote na kuhakikisha mauaji hayo yanakomeshwa mara moja. 

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa vile vile amesema kuwa, katika hali ambayo dunia imeshindwa kuzuia kutokea mauaji ya watu wasio na hatia huko Palestina, ni wajibu wa pande zote kuingia haraka kwenye utekelezaji wa kusimamisha vita. Kila upande unapaswa kuweka chini silaha mara moja na milele ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia.

Volker Türk

Baada ya kupita siku 311 tangu baada ya utawala ghasibu wa Israel unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu kuanzisha vita vya maangamizi ya kimbari  dhidi ya wananchi wa Gaza, ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imewasilisha takwimu za kutisha za jinai za kivita za utawala huo ghasibu na mauaji ya raia wa Palestina.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, zaidi ya jinai 3,486 zimefanywa na Wazayuni katika kipindi cha miezi 10 iliyopita huko Gaza ambapo kutokana na jinai hizo, zaidi ya Wapalestina 49,897 wameuawa shahidi au kutoweka, ambapo hatima ya takriban watu elfu 10 haijulikani huku miili ya mashahidi zaidi ya 39,897 ikiwa imetambuliwa katika hospitali mbali mbali za ukanda huo.