Hamas: Usitishaji mapigano lazima uhusishe kuondoka kikamilifu Israel Ukanda wa Gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kwa mara nyingine tena imesisitiza kuwa makubaliano yoyote na Israel lazima yahakikishe usitishaji kamili wa vita huko Gaza, kuondoka kikamili majeshi ya Israel katika eneo hilo na makubaliano ya kubadilishana wafungwa.
Hamas ilisema katika taarifa yake Alhamisi ya jana kwamba makubaliano hayo yanapaswa pia kurahisisha kurejea kwa Wapalestina waliokimbia makazi yao na kulijenga upya eneo lililoharibiwa la Ukanda wa Gaza.
Afisa wa Hamas, Hossam Badran, amesema katika taarifa hiyo kwamba harakati hiyo inatazama mazungumzo yanayoendelea huko Doha kuhusu kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa kwa mtazamo wa kimkakati unaolenga kukomesha uvamizi wa Israel Ukanda wa Gaza.
"Hamas inaamini kwamba mazungumzo yoyote lazima yazingatie mpango wa wazi wa kutekeleza kile kilikubaliwa hapo awali. Kikwazo cha kufikiwa usitishaji vita katika eneo la Gaza ni kuendelea ukwepaji wa 'Israeli wa kutekeleza makubaliano hayo," Badran aliongeza.
Hossam Badran amesema: "Makubaliano yoyote lazima yaafiki usitishaji vita kamili, kuondoka kabisa Waisraeli kutoka Gaza, kurejea wakimbizi katika makazi yao, pamoja na makubaliano ya kubadilishana wafungwa."
Taarifa hiyo inakuja wakati duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano ikiendelea huko Doha, ambapo Hamas imeamua kwamba haitashiriki.
Hamas imewataka wapatanishi kutekeleza makubaliano ya suluhu yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa badala ya kufanya mazungumzo ya kufikia mapatano mapya.
Sambamba na mazungumzo hayo, Israel inaendeleza mauaji ya kimbari huko Gaza na ripoti zinaonyesha kuwa, zaidi ya Wapalestina 40,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 92,400 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.