Hizbullah: Hakuna shaka tutatoa jibu kwa mauaji ya kigaidi ya Israel
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena imesisitiza azma yake ya kulipiza kisasi cha mauaji ya Israel dhidi ya kamanda mwandamizi wa kundi hilo la Mapambano ya Kiislamu, licha ya juhudi za Marekani za kuukingia kifua utawala huo wa Kizayuni na kutaka kuuepusha na matokeo mabaya ya jinai zake.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika mahojiano na mtandao wa televisheni ya al-Manar ya Lebanon na kuongeza kuwa, "Jibu ni uamuzi na uamuzi huu utafanyika bila shaka inshaAllah."
Amesisitiza kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa Hizbullah italipiza kisasi cha damu ya Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wakuu wa kundi hilo, na Ismail Haniyah, aliyekuwa kiongozi kisiasa wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), ambao waliuawa katika operesheni tofauti za kigaidi zilizofanywa na Tel Aviv katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut na mji mkuu wa Iran, Tehran, mwishoni mwa mwezi uliopita.
Sheikh Qassim ameielezea ziara ya mjumbe wa Marekani, Amos Hochstein nchini Lebanon, ambayo inadaiwa ililenga kupunguza mvutano kati ya Israel na Hizbullah kama "onyesho" katika "mzunguko mbaya", akibainisha kuwa afisa huyo wa Washington hakuwasilisha "mapendekezo mahususi ya Marekani."
Juzi Jumatano, Hochstein alidai kuwa anaamini vita kamili kati ya Israel na Hizbullah vinaweza kuepukika na kuongeza kuwa, makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza pia yatasaidia kuzuia kuzuka kwa vita vikubwa zaidi.
Kwingineko katika matamshi yake, Sheikh Naim Qassim amebainisha kuwa, ushindi wa Lebanon dhidi ya adui Mzayuni katika vita vya Julai 2006 "sio tukio la kipekee", bali lilikuwa "chaguo ambalo liligeuka kuwa msingi wa siku zijazo."