Israel yaendelea kufanya mashambulio ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza
Mashambulio ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yameendelea kuripotiwa.
Wapalestina kadhaa wameripotiwa kuuawa shahidi katika kipindi cha saa 24 zilizopita kufuatia mashambulio ya anga ya jeshi la Israel huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.
Katika upande mwingine, Wapalestina wasiopungua 21, akiwemo mama na watoto wake sita, waliuawa shahidi jana wakati jeshi la utawala haramu wa Israel liliposhambulia maeneo kadhaa katika Ukanda wa Gaza.
Mashambulio ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza yangali yanaendelea huku takwimu zikionyesha kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa ikiwa imeshapindukia elfu arubaini.

Utawala wa Kizayuni umeendelea kukaidi kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mara moja mapigano, huku ukiandamwa na shutuma za kimataifa kwa kuendeleza mashambulizi ya kikatili na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza uliyoanzisha Oktoba 7 mwaka jana.
Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kwa mara nyingine tena imesisitiza kuwa makubaliano yoyote na Israel lazima yahakikishe usitishaji kamili wa vita huko Gaza, kuondoka kikamili majeshi ya Israel katika eneo hilo na makubaliano ya kubadilishana wafungwa.