Israel yaendeleza ukatili, yaua Wapalestina 50 ndani ya saa 24 Gaza
Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza imesema Wapalestina wasiopungua 50 wameuawa shahidi na wengine 124 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo mbali mbali ya Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita.
Jeshi la Kizayuni limeamuru kuhamishwa kwa wanajeshi wapya kutoka maeneo ya Deir el-Balah karibu na Khan Younis, katikati mwa Gaza, kuashiria upanuzi wa operesheni za ardhini za jeshi hilo kutoka kusini hadi katikati mwa Gaza.
Habari zaidi zinasema kuwa, jeshi la Israel limeua takriban wakulima 40 katika eneo la Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, katika mashambulizi ya anga. Aidha jana Jumanne, mashambulizi ya Israel dhidi ya Shule ya Mustafa Hafez inayohifadhi wakimbizi wa Kipalestina magharibi mwa Ukanda wa Gaza yaliua takriban raia 20 na kujeruhi wengine wengi.
Mashambulio hayo ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza yangali yanaendelea huku takwimu zikionyesha kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa ikiwa imeshapindukia 40,000.

Utawala wa Kizayuni umeendelea kukaidi kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mara moja mapigano, huku ukiandamwa na shutuma za kimataifa kwa kuendeleza mashambulizi ya kikatili na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7 mwaka jana.
Wakati huo huo, utawala katili wa Israel umemuua Khalil al-Muqdah, kamanda katika Brigedi ya Mashahidi wa Al-Aqsa, katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani dhidi ya gari lililokuwa limebeba huko Sidon nchini Lebanon, yapata kilomita 40 kusini mwa Beirut.